Nigeria yalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127566-nigeria_yalaani_mashambulizi_ya_israel_dhidi_ya_iran
Nigeria imelaani vikali mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran na kusema uhasama huo wa Israel utatumbukiza eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) katika hali ya taharuki.
(last modified 2025-06-15T01:06:04+00:00 )
Jun 15, 2025 01:06 UTC
  • Nigeria yalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran

Nigeria imelaani vikali mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran na kusema uhasama huo wa Israel utatumbukiza eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) katika hali ya taharuki.

“Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria inalaani shambulizi lililofanywa na Israel dhidi ya Iran, ambalo limechochea kuongezeka kwa uhasama kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Israel,” ilmesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumamosi.

Imesema: “Muendelezo wa mashambulizi ya kisasi siyo tu kwamba unaweka maisha ya raia katika hatari, bali pia unatishia kulizamisha eneo pana la Mashariki ya Kati katika hali ya taharuki zaidi."

Nigeria pia imetoa wito kwa suluhisho la kidiplomasia kwa mzozo huu unaoendelea.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuongeza juhudi za kuleta utulivu wa haraka na kutoa jukwaa la mazungumzo ya maana.”

Taarifa hiyo inakuja siku moja tu baada ya Umoja wa Afrika kueleza wasiwasi mkubwa kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, ametoa tamko la “wasiwasi mkubwa kuhusiana na mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Iran na kuongezeka uhasama katika eneo la Mashariki ya Kati.”

Afrika Kusini pia imetoa taarifa ikilaani vikali hujuma ya Israel dhidi ya Iran. Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini (DIRCO) imesema katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa usiku kwamba: "Afrika Kusini inaelezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na Israel ndani ya Iran tarehe 13 Juni 2025, ikiwa ni pamoja na athari za mashambulizi hayo kwenye maeneo ya kijeshi, vituo vya nyuklia na miundombinu ya kiraia. Ripoti za raia kujeruhiwa pamoja na wanajeshi, zinasumbua sana."

"Hatua hizi zinazua wasiwasi mkubwa mbele ya sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na sheria za uhuru, uadilifu na ulinzi wa raia zilizoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa za kibinadamu," imesema sehemu nyingine ya taaarifa ya idara hiyo ya Afrika Kusini.

Wakati ikitoa salamu zake za rambirambi kwa serikali ya Iran na familia za watu wote waliouawa shahidi katika hujuma ya kigaidi ya Israel; Afrika Kusini pia imetilia mkazo msimamo wake usioyumba wa kutatuliwa kwa amani mizozo yote.