MSF: Unyanyasaji wa kijinsia umeongezeka mashariki mwa DRC
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetangaza kuwa, vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vimeongezeka mno katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika ripoti iliyochapishwa wiki hii, shirika hilo limeonyesha wasiwasi wake kuhusu hali ambayo imezorota kwa kasi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kutishwa na ongezeko kubwa la unyanyasaji wa kingono lililorekodiwa, haswa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini, tangu mwanzoni mwa mwaka.
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetoa tahadhari tena kuhusu unyanyasaji wa kingono nchini DRC, hasa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini, ambayo inakabiliwa na mzozo mkali kati ya kundi la AFC/M23 linaloungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, na jeshi la Kongo na washirika wake. Hali hi inatia wasiwasi hasa katika mikoa hii miwili ya mashariki mwa nchi, ambapo kumekuwa na ongezeko la kutisha la ukatili wa kijinsia tangu mwanzoni mwa mwaka wa 2025, MSF inaandika katika ripoti iliyochapishwa wiki hii.
MSF pia inasema kwamba imeona hali inayozidi kuzorota katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ikionyesha hasa kesi 40,000 ilizoshughulikia mwaka 2024 huko Kivu Kaskazini pekee—idadi ambayo haijawahi kushuhudiwa, shirika hilo linasema. Kwa mwaka wa 2025, MSF inadai kuwa tayari imerekodi wahasiriwa 7,400 huko Goma, 2,400 huko Saké, na 700 huko Kivu Kusini. Idadi kubwa ya unyanyasaji huu wa kijinsia hufanywa na watu wenye silaha na huathiri zaidi wanawake, lakini pia kwa watoto: karibu 13% ya wahasiriwa ni watoto wadogo, shirika hilo linabainisha.