Amnesty Kenya: Vifo 16 vimesajiliwa kufuatia ghasia zilizojiri nchini
(last modified Thu, 26 Jun 2025 15:50:29 GMT )
Jun 26, 2025 15:50 UTC
  • Amnesty Kenya: Vifo 16 vimesajiliwa kufuatia ghasia zilizojiri nchini

Watu 16 wameuawa na mamia wamejeruhiwa wakati wa maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali nchini Kenya siku ya Jumatano, ambapo kwa mujibu wa Mkuu wa shirika la Amnest Kenya na Kamisheni ya Taifa ya Kenya ya Haki za Binadamu, wengi wao wameuawa na polisi.

Haya yamejiri mwaka mmoja baada ya kushuhudiwa maandamano ya machafuko makubwa ya kupinga muswada wa ushuru yaliyofikia kilele chake kwa kushambuliwa jengo la Bunge.

Duru za ndani na shirika la habari la Reuters zimeripoti kuwa, maelfu ya Wakenya siku ya Jumatano walijitokeza barabarani kuadhimisha maandamano ya mwaka jana nchini humo, ambapo zaidi ya watu 60 walipoteza maisha, huku polisi wakifyatua mabomu ya kuta machozi na kuwanyunyizia waandamanaji maji ya kuwasha ili kuwatawanya katika mji mkuu, Nairobi.

Baadhi ya watu walioandamana Jumatano hii katika mji mkuu Nairobi walionekana wakipeperusha bendera ya Kenya na mabango yenye picha za waandamanaji waliouawa mwaka jana na kuimba: "Ruto lazima Aondoke".

Maandamano ya maelfu ya Wakenya Jumatano wiki hii yamefanyika kukumbuka maandamano ya mwaka jana yaliyoongozwa na vijana wa kizazi kizazi kipya (Gen Z) kupinga ongezeko la kodi, ambapo watu wasiopungua 60 waliuawa na askari vya usalama. Ripoti hii ni kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu.