Museveni achukua fomu ya kuwania muhula wa saba madarakani
(last modified Sun, 29 Jun 2025 02:44:41 GMT )
Jun 29, 2025 02:44 UTC
  • Museveni achukua fomu ya kuwania muhula wa saba madarakani

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameomba tena uteuzi wa kugombea muhula wa saba, hatua inayomuelekeza kwenye miaka 50 ya kuwa madarakani.

Rais Museveni, mwenye umri wa miaka 80, amepuuza wito wa kustaafu huku wakosoaji wake wakionya kwamba amegeuka kuwa mtawala wa kiimla, kwa kuwa hana upinzani wa maana hata ndani ya chama tawala cha National Resistance Movement (NRM).

 Museveni alipokelewa na umati mkubwa wa wafuasi alipokwenda kuchukua fomu za uteuzi katika makao makuu ya chama jijini Kampala. Museveni alichukua madaraka kwa mara ya kwanza kama kiongozi wa waasi mwaka 1986, na tangu hapo ameshinda uchaguzi mara sita, ingawa chaguzi za hivi karibuni zimegubikwa na vurugu na madai ya wizi wa kura.

Mpinzaniwake mkuu katika uchaguzi uliopita Robert Kyagulanyi, al-maarufu Bobi Wine pia ametangaza nia ya kugombea katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari 2026.

Tangu kupata uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1962, Uganda haijawahi kushuhudia mabadiliko ya uongozi kwa njia ya amani.

Museveni, mmoja wa marais wa nne barani Afrika walioongoza kwa muda mrefu zaidi, amekuwa akishutumiwa na upinzani na makundi ya kutetea haki za binadamu kuwa anatumia jeshi kuwadhoofisha wapinzani wake kwa kutoa vitisho, vipigo au kuwasweka jela.

Mwaka jana (2024) Rais Museveni alimteua mwanawe wa kiume, Jenerali Muhoozi Kainerugaba kuwa Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.