Ajali mbaya ya barabarani yaua watu 38 nchini Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127762-ajali_mbaya_ya_barabarani_yaua_watu_38_nchini_tanzania
Watu 38 wameripotiwa kufariki dunia na wengine 30 wamejeruhiwa nchini Tanzania baada ya mabasi mawili kugongana na kuwaka moto.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jun 30, 2025 00:54 UTC
  • Ajali mbaya ya barabarani yaua watu 38 nchini Tanzania

Watu 38 wameripotiwa kufariki dunia na wengine 30 wamejeruhiwa nchini Tanzania baada ya mabasi mawili kugongana na kuwaka moto.

Ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Channel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitokea Same, ambapo magari hayo yaligongana uso kwa uso na kushika moto.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba kutokana na athari za moto huo, hadi sasa miili 36 bado haijatambulika.

Ameongeza kuwa, kutokana na hali ya miili ya marehemu kuungua vibaya, serikali imeanza taratibu za uchunguzi wa vinasaba (DNA) kusaidia kuwatambua marehemu, huku wananchi wakihimizwa kufuatilia taarifa za wapendwa wao waliopotea ili kusaidia zoezi hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ameeleza kuwa chanzo cha ajali ni kupasuka kwa tairi la mbele la basi la Channel One, lililosababisha basi hilo kupoteza mwelekeo na kugongana na Coaster kabla ya magari hayo kushika moto.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema ajali hiyo ni tukio la majonzi makubwa ambalo halijawahi kushuhudiwa katika mkoa huu, akifafanua kuwa majeruhi 24 wamelazwa katika Hospitali ya Mji Same, huku watano wakiwa katika Hospitali ya Mawenzi na KCMC kwa matibabu zaidi. Katika taarifa iliyotolewa jana, Rais Samia Suluhu Hassan ameelezea masikitiko makubwa na kutuma salamu za rambirambi.

Sambamba na ujumbe wake wa salamu za pole na rambirambi, Rais Samia ametoa wito wa umakini kwa madereva na kuheshimu sheria za barabarani.

Ajali mbaya za barabarani hutokea mara kwa mara nchini Tanzania.  Katika ripoti ya mwaka 2018, Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa mnamo mwaka 2016, watu 13,000 hadi 19,000 nchini Tanzania walikufa katika ajali za barabarani, idadi iliyokinzana na ile ya serikali iliyoorodhesha vifo 3,256.