Gachagua aonywa huwenda akashtakiwa ikibainika alihusika na ghasia za maandamano
-
Rigathi Gachagua
Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua atakamatwa na kushtakiwa kama Mkenya mwengine yeyote iwapo ushahidi utamhusisha na ghasia zilizoshuhudiwa nchini humo mnamo Juni 25. Hayo ni kwa mujibu wa Idara ya Upelelezi ya Kenya (DCI).
Mkuu wa DCI, Mohamed Amin amesema kuwa hakuna mwanasiasa ambaye ana kinga ya kukamatwa wakati serikali inapoendelea kuwasaka waliofadhili maandamano ya wiki iliyopita.
Ghasia, mauaji na uharibifu wa mali ulishuhudiwa wakati wa maandamano hayo yaliyofanyikka kuadhimisha mwaka mmoja tangu Gen Z wavamie Bunge la Kitaifa mnamo Juni 25, 2024.
Mohamed Amin amesema: “Kuhusiana na Rigathi, ningependa kuweka mambo bayana kuwa hana kinga yoyote ya kutoshtakiwa. Yeye ni kama Mkenya mwengine ambaye yuko chini ya sheria za nchi.”
Ameongeza kuwa: “Iwapo uchunguzi utabaini aliihusika na kupanga ghasia, fujo na uharibifu uliotokea, basi sheria itachukua mkondo wake dhidi yake.”
Takwimu zilizotolewa na serikali kupitia Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, zilisema watu 10 walifariki dunia katika maandamano hayo.
Hata hivyo, mashirika ya kijamii kama Shirika la Amnesty International yanasema idadi hiyo ilifikia watu 16.
Mkuu huyo wa DCI amesema kuwa kufikia sasa, uchunguzi wao umeonyesha kuwa ghasia hizo kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Nairobi, zilikuwa zimepangwa.