Sudan yalaani vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128552
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imeshutumu vikwazo vipya vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya watu binafsi na mashirika ya Sudan, na kusisitiza kuwa havina "viwango vya uadilifu vya kisheria."
(last modified 2025-07-21T02:44:51+00:00 )
Jul 20, 2025 14:07 UTC
  • Sudan yalaani vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi yake

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imeshutumu vikwazo vipya vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya watu binafsi na mashirika ya Sudan, na kusisitiza kuwa havina "viwango vya uadilifu vya kisheria."

"Haiwezekani kufananisha" Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na "makundi ya waasi yaliyoharamishwa," imesema taarifa ya wizara hiyo, ikiitaka EU kuchukua mtazamo wenye mlingano zaidi ambao unazingatia hali ya kipekee ya kitaifa ya Sudan.

Siku ya Ijumaa, EU ilipasisha vikwazo dhidi ya watu wawili na mashirika mawili yenye uhusiano na jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), ikijumuisha kufungia mali zao, kupiga marufuku utoaji wa fedha au rasilimali za kiuchumi, kwa njia ya moja kwa moja au isiyo moja kwa moja, na vile vile marufuku ya kusafiri.

Haya yanajiri siku chache baada ya Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kuripotiwa kuua karibu watu 300 katika wimbi jipya la mashambulizi katika jimbo la Kordofan Kaskazini, magharibi mwa nchi.

Mapigano makali kati ya jeshi la kitaifa la Sudan na waasi wa RSF yaliyoanza mwezi Aprili 2023 yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 na kuwafanya watu milioni 14 kuhama makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za ndani nchini Sudan.

Hata hivyo, tafiti huru zinaonyesha kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe inaweza kupindukia watu 130,000.