Wanahabari Nigeria walaani mauaji ya waandishi wenzao huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129658-wanahabari_nigeria_walaani_mauaji_ya_waandishi_wenzao_huko_gaza
Muungano wa Waandishi wa Habari wa Nigeria (NUJ) umelaani vikali mauaji ya wanahabari yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel huko Gaza na kusisitiza kuwa, hujuma hizo za utawala wa Kizayuni dhidi ya waandishi wenzao katu haziwezi kuwazuia wahudumu wa tasnia hiyo kuendelea kufichua ukweli.
(last modified 2025-08-18T06:43:03+00:00 )
Aug 18, 2025 06:43 UTC
  • Wanahabari Nigeria walaani mauaji ya waandishi wenzao huko Gaza

Muungano wa Waandishi wa Habari wa Nigeria (NUJ) umelaani vikali mauaji ya wanahabari yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel huko Gaza na kusisitiza kuwa, hujuma hizo za utawala wa Kizayuni dhidi ya waandishi wenzao katu haziwezi kuwazuia wahudumu wa tasnia hiyo kuendelea kufichua ukweli.

Rais wa NUJ, Alhassan Yahaya Abdul amelaani mauaji hayo ya waandishi wa habari huko Gaza, na kuyataja kuwa "ukiukaji kamili wa sheria za kimataifa." Amesema zaidi ya waandishi wa habari 274 wameripotiwa kuuawa katika maeneo mbali mbali ya Ukanda wa Gaza kutokana na hujuma za kijeshi za Israel.

Kadhalika NUJ imeeleza kuwa, uandishi wa habari si uhalifu na kusisitiza kwamba, jinai hizo za Wazayuni kamwe hazitavifumba mdomo vyombo vya habari.
Aidha umoja huo wa wanahabari nchini Nigeria umetoa wito kwa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa kuchunguza uhalifu huo Israel huko Gaza.

Rais wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Nigeria amesisitiza kuwa, amani inaweza kupatikana tu kwa njia ya mazungumzo na haki, na wala sio kupitia vurugu, ghasia na mabavu.

Abdul ameliambia shirika la habari la Iran Press mjini Abuja kuwa, "Kuua waandishi wa habari hakutazuia waandishi wa habari kufanya kazi yao, na kamwe hakutazuia uandishi wa habari kuendelea."

"Hatua za Israeli zinakwenda kinyume na sheria na mikataba ya kimataifa. Tunalaani vitendo kama hivyo kwa jumla," amesisitiza kiongozi huyo wa wanahabari Nigeria.