ADF yanyooshewa kidole cha lawama kwa mauaji mapya ya Kivu Kaskazini
-
Kundi la ADF ni maarufu kwa vitendo vyake vya uhalifu na jinai katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.
Waasi wa ADF wameongeza mashambulizi dhidi ya raia katika siku za hivi karibuni mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Jumapili ya jana, Agosti 17, watu wasiopungua tisa waliuawa katika mji wa Oicha, makao makuu ya eneo la Beni, kulingana na vyanzo vya afya na utawala vya eneo hilo.
Mashirika ya kiraia ya eneo hilo yamesema kuwa, shambulio hilo lililotokea Agosti 17 mashariki mwa DRC, hasa katika mji wa Oicha, lilifanyika katika kitongoji cha Mbimbi. Raia waliovamiwa majumbani mwao walipigwa risasi na kufa, na miili mingine ilipatikana ikiwa imechomwa moto wakati wa shambulio hilo.
Takriban nyumba ishirini zilichomwa moto na washambuliaji. Miili ya wahasiriwa ilipelekwa katika hospitali ya Oicha, mji ulioko takriban kilomita kumi na tano kaskazini mwa Beni katikamkoa wa Kivu Kaskazini.
Jeshi la Kongo, ambalo limelaani shambulio hili, linadai kuwa ADF inajaribu kuwavuruga FARDC kutokana na hatua zilizochukuliwa na jeshi dhidi ya kundi hili la waasi.
Kulingana na jeshi, ADF imeamua kulipiza kisasi kwa raia. Wiki iliyopita, takriban watu 47 waliuawa na ADF katika eneo la Lubero, kulingana na ripoti mpya kutoka kwa mamlaka, licha ya operesheni za pamoja kati ya FARDC na vikosi vya Uganda katika eneo hilo.
Kundi la ADF ni maarufu kwa vitendo vyake vya uhalifu na jinai katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri ambayo yamezingirwa na jeshi la Kongo tangu mwezi Mei 2021, huku maafisa kijeshi na polisi wakichukua nafasi za utawala kutoka kwa raia.