Ripoti: Israel imepatwa na mshtuko wa kiuchumi wa vita na Iran
Ripoti ya vyombo vya habari vya Israel imefichua changamoto zinazoukabili utawala huo baada ya vita vya siku 12 na Iran mwezi Juni mwaka huu,na kubainisha kuwa uchumi wa Israel umedorora sana, na kushuka kwa viashiria vya jumla, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa pato la taifa (GDP), uwezo wa manunuzi na uwekezaji.
Calcalist ambalo ni gazeti la masuala ya biashara na uchumi na pia ni tovuti limeandika kuwa vita vya karibuni kati ya Israel na Iran vimerudisha nyuma uchumi wa utawala huo kwa mwaka mmoja na kusababisha ukuaji hasi katika robo ya pili ya mwaka huu.
Ripoti hiyo ilitaja data rasmi kutoka kituo cha takwimu cha serikali, ikionyesha kupungua pakubwa kwa Pato la Taifa kwa asilimia 3.5 ikilinganishwa na robo ya awali ya mwaka huu
Ripoti ya gazeti la Calcalist imeongeza kuwa, sekta ya biashara ndiyo iliyoathiriwa zaidi, ambayo ilikabiliwa na kushuka kwa asilimia 7 ya pato lake.
Uchumi wa Israel ulikuwa umedorora tangu utawala wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu uanzishe vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza, lakini vita vya kichokozi ulivyovianzisha dhidi ya Iran katikati ya mwezi wa Juni mwaka huu vimeugharimu utawala huo takriban dola bilioni 6.