Kwa nini maandamano yameshadidisha hali mbaya ya mgogoro Israel?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129714-kwa_nini_maandamano_yameshadidisha_hali_mbaya_ya_mgogoro_israel
Mgogoro wa hivi sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na kushadidi maandamano yanaashiria kudhoofika muundo wa kisiasa na kiusalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2025-08-19T10:32:13+00:00 )
Aug 19, 2025 10:26 UTC
  • Maandamano ya kupinga sera za Benjamin Netanyahu
    Maandamano ya kupinga sera za Benjamin Netanyahu

Mgogoro wa hivi sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na kushadidi maandamano yanaashiria kudhoofika muundo wa kisiasa na kiusalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa, waandamanaji walifunga barabara katika maeneo mengi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Walowezi hao wa Israel waliokuwa wakiandamana walifunga mitaa ya Quds inayokaliwa kwa mabavu na Tel Aviv wakipinga maamuzi ya serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ya kuendeleza vita Gaza na kutaka kufikiwa makubaliano ya kubadilishana mateka kwa ajili ya kuachiliwa huru mateka wa Israel huko Gaza.

Wito wa familia za wafungwa wa Kizayuni uliwavuta mamia ya wakaazi wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kwenye mitaa ya Tel Aviv na miji mingine. Kwa kuziba barabara na kufanya mikusanyiko mikubwa, waandamanaji hao walitaka kukomeshwa kwa vita vya Gaza, kubadilishana mateka na kupinduliwa kwa baraza la mawaziri la Netanyahu.

Maandamano na migomo ya maeneo yote iliyoitishwa na familia za mateka wa Kizayuni dhidi ya vita vya Ghaza imewakasirisha mawaziri kadhaa wenye misimamo mikali katika baraza la mawaziri la utawala huo ghasibu. Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni amelaani maandamano hayo na kusema: "migomo ya leo inaidhoofisha Israel, linaipa nguvu Hamas na kuchelewesha kurejea kwa mateka."

Yair Golan, kiongozi wa Chama cha Kidemokrasia cha Kizayuni, pia alitangaza wakati wa mgomo mkuu kwamba fursa zinakimbia na kwamba juhudi zote zinapaswa kufanywa "kuwarudisha mara moja mateka."

Maandamano ya kupinga sera za Benjamin Netanyahu

 

Gadi Eisenkot, Mkuu wa zamani wa Majeshi ya Israel na mmoja wa viongozi wa upinzani alimkosoa vikali Benjamin Netanyahu na kueleza kuwa, hana uwezo wa kuongoza na kuwajibika na kwamba, anaweka kando maamuzi magumu ya kutanguliza maslahi yake binafsi na kisiasa badala ya yale ya utawala ghasibu wa Israel; na kwamba vitendo hivi vinaupeleka utawala huo shimoni.

Kuongezeka kwa maandamano katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kumekuwa na madhara makubwa ya kisiasa na kiusalama. Waandamanaji wengi wanalichukulia baraza la mawaziri la Netanyahu kwamba, limekosa mpango na uwezo wa kusimamia vita vya Gaza na kuachiliwa kwa mateka. Hitilafu kali kati ya ngazi za kisiasa, kijeshi na kiusalama za utawala wa Kizayuni nazo zimefikia kiwango kipya.

Majenerali wastaafu na makamanda wa zamani wamekosoa sera za vita za serikali, na wengine wametoa wito wa kukomeshwa vita vya Gaza. Kuendelea kwa maandamano na kutoridhika kwa umma pia kumeongeza uwezekano wa mapigano ya mitaani na uasi mkubwa.

Operesheni za muqawama wa Palestina katika miaka ya hivi karibuni pia zimekuwa na taathira kubwa katika kushadidi maandamano ya ndani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Wakiwa na nara kama vile "komesha vita" na "waachilie huru mateka," waandamanaji wamekiri vilivyo kwamba utawala wa Kizayuni umeshindwa kufikia malengo yake katika vita vya Gaza.

Operesheni za Wanamuqawama wa Palestina zimemfanya Netanyahu akabiliwe na mashinikizo ya ndani

 

Muqawama wa Palestina ukiwa na nguvu na mshikamano usio na kifani, umeuwekea mashinikizo utawala wa Kizayuni katika nyanja za kijeshi na kisiasa. Shinikizo hili limesababisha kushadidi mno hitilafu ndani ya baraza la mawaziri na miongoni mwa vyama vya upinzani, na kuzidisha maandamano na malalamiko dhidi ya sera za Netanyahu.

Maandamano yenye wigo mpana dhidi ya serikali ya Netanyahu yanaonyesha kuwa, wakaazi wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) hawana imani tena na sera za kivita na usalama za Tel Aviv. Mgawanyiko kati ya vyama, kujiuzulu kwa maafisa wa usalama, na mizozo na hitlafu ndani ya baraza la mawaziri ni miongoni mwa ishara za mgogoro kupinga uhalali wa serikali ya Netanyahu.

Mgogoro wa sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu unaakisi kudhoofika muundo wa kisiasa na kiusalama wa utawala wa Kizayuni. Muqawama wa Wapalestina, kwa kutumia nguvu ya kijeshi, vyombo vya habari, na nguvu ya wananchi, umeweza kubadilisha mlingano wa nguvu.

Kwa kuzingatia kushadidi maandamano na kushindwa Netanyahu kutekeleza ahadi zake kuhusiana na vita vya Gaza, mwenendo wa kutoridhika utaongezeka, na viongozi wa utawala huo wa Kizayuni wanakabiliwa na hali mbaya ambayo wao ndio sababu kuu ya kutokea kwake.