Iran yalaani uamuzi wa Israel wa kuwafurusha Wapalestina Jiji la Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129664-iran_yalaani_uamuzi_wa_israel_wa_kuwafurusha_wapalestina_jiji_la_gaza
Iran imelaani vikali uamuzi wa Israel wa kuwalazimisha Wapalestina kuhama makazi yao na kuelekea kusini mwa Gaza na kusisiitiza kuwa, jamii ya kimataifa na nchi za Kiislamu zina wajibu wa kukabiliana na uhalifu huo wa kutisha wa kivita.
(last modified 2025-08-18T03:15:59+00:00 )
Aug 18, 2025 03:15 UTC
  • Iran yalaani uamuzi wa Israel wa kuwafurusha Wapalestina Jiji la Gaza

Iran imelaani vikali uamuzi wa Israel wa kuwalazimisha Wapalestina kuhama makazi yao na kuelekea kusini mwa Gaza na kusisiitiza kuwa, jamii ya kimataifa na nchi za Kiislamu zina wajibu wa kukabiliana na uhalifu huo wa kutisha wa kivita.

Katika taarifa yake jana Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kuwa, hatua ya Israel kuwatimua kwa lazima wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na wakati huo huo kutekeleza mpango wake unaoitwa "Israel Kubwa Zaidi" unadhihirisha hatari ya utawala huo kwa amani na usalama wa kieneo na kimataifa.

Wizara ya Mambo ya Nje imesema kuwafurusha kwa lazima wakazi wa Gaza kunalenga kuharibu kabisa utambulisho wa kitaifa wa Wapalestina katika Ukanda huo na kukamilisha mauaji ya kimbari.

Imebainisha kuwa, wakazi wa Jiji la Gaza wamekuwa katika mashambulizi makali zaidi kwa takriban miaka miwili na kukabiliwa na baa la njaa lililowekwa na utawala wa Israel katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

"Uamuzi wa utawala ghasibu wa kuwahamisha wakazi wa Jiji la Gaza kwa lazima...ni mfano wa wazi wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, ambao hauna lengo lolote ila kukamilisha mpango wa mauaji ya halaiki na kuifuta Palestina kama taifa na utambulisho wake," wizara hiyo imesisitiza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema maamuzi hayo ni natija ya kutoadhibiwa viongozi watenda jinai wa Israel, uungaji mkono kamili wa kijeshi na kisiasa wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kwa utawala huo ghasibu, na kutochukua hatua kali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mahakama za kimataifa za kuwafungulia mashitaka viongozi hao wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Iran inatahadharisha dhidi ya njama za utawala ghasibu wa Israel za kushadidisha mauaji ya Wapalestina na kufanya jinai zaidi kwa kisingizio cha kuwahamisha watu wa Jiji la Gaza kupelekwa kusini mwa Ukanda huo.