Iran yaonya: Israel itajitanua zaidi Asia Magharibi iwapo haitadhibitiwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129682-iran_yaonya_israel_itajitanua_zaidi_asia_magharibi_iwapo_haitadhibitiwa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baqaei amesema Israel ni tishio kwa usalama na uthabiti wa Asia Magharibi kutokana na mwenendo wake wake kupenda kujitanua, akionya kuwa eneo hili la kistratejia linaweza kukabiliwa na vita visivyoisha ikiwa utawala huo hautazuiwa.
(last modified 2025-09-22T12:23:50+00:00 )
Aug 18, 2025 11:04 UTC
  • Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baqaei.
    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baqaei.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baqaei amesema Israel ni tishio kwa usalama na uthabiti wa Asia Magharibi kutokana na mwenendo wake wake kupenda kujitanua, akionya kuwa eneo hili la kistratejia linaweza kukabiliwa na vita visivyoisha ikiwa utawala huo hautazuiwa.

Baqaei amesema hayo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran leo Jumatatu na kuongeza kuwa, utawala huo ghasibu hauna mipaka ikija kwa malengo yake ya kujitanua.

"Ukweli ni kwamba, kwa nchi za kieneo, wakati huu kuliko wakati wowote mwingine, tabia ya kujitanua na ubabe wa utawala wa Israel imedhihirika wazi," amesema Baqaei na kuongeza kuwa, matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambapo anadai kuwa na jukumu la kutekeleza mpango wa "Israel Kubwa Zaidi" ambayo inajumuisha sehemu kubwa ya ardhi za Waarabu na Waislamu, yanadhihirisha kuwa utawala wa Israel hauna mipaka katika suala la kujitanua.

Ameongeza kuwa, kuendelea kwa mauaji ya halaiki ya Israel katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan sambamba na kumezea mate ardhi za Jordan, Syria, Lebanon na hata sehemu kubwa ya Saudi Arabia, kunaonyesha wazi kuwa utawala huo unatishia usalama na uthabiti wa eneo hili.

"Ikiwa upanuzi huu hautadhibitiwa, eneo letu (la Asia Magharibi) bila shaka litakabiliwa na vita visivyo na mwisho," mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesisitiza.

Katika taarifa yake jana Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema kuwa, hatua ya Israel kuwatimua kwa lazima wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na wakati huo huo kutekeleza mpango wake unaoitwa "Israel Kubwa Zaidi" kunadhihirisha hatari ya utawala huo kwa amani na usalama wa kieneo na kimataifa.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa na hususan nchi za Kiislamu zina wajibu wa kukabiliana na uhalifu huo wa kutisha wa kivita wa utawala pandikizi wa Israel.