Ugonjwa wa kipindupindu wauwa watu 63 mashariki mwa Chad
Watu wasiopungua 63 wamepoteza maisha kwa ugonjwa wa kipindupindu katika jimbo la Ouaddai mashariki mwa Chad tangu katikati ya mwezi Julai mwaka huu. Taraifa hii imetolewa na Wizara ya Afya ya nchi hiyo.
Dk. Abdel-Mahmoud Chene, mjumbe wa Afya ya Umma na Kinga katika jimbo la Ouaddai, amesema katika mkutano ulioongozwa na Waziri wa Afya ya Umma wa Chad, Abdelmadjid Abderahim, kwamba tangu kesi ya kwanza iliporipotiwa Julai 13 mwaka huu jumla ya watu 938 wanaoshukiwa kuugua kipindupindu wamesajiliwa, huku sampuli 52 zikifanyiwa uchunguzi wa kimaabara.
Kipindupindu ni ugonjwa unaoambukiza haraka unaosababishwa na bakteria vibrio cholerae na kimsingi huambukizwa kupitia maji machafu. Ugonjwa huo husababisha upungufu wa maji mwilini haraka na baadaye kifo, ikiwa hautatibiwa haraka. Matibabu ni pamoja na dawa aina ya antibiotics na drip ili kurejesha maji mwilini.
Mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) lilitahadharisha kuwa watoto elfu themanini wako katika hatari kubwa ya kupatwa na kipindupindu kufuatia kuanza kwa msimu wa mvua magharibi na katikati mwa Afrika.
Watoto, khususan wale wenye umri chini ya miaka mitano wako katika hatari ya kupata kipindupindu kutokana na sababu kama vile usafi duni, ukosefu wa vyoo na maji salama, na upo uwezekano mkubwa wa kupungukiwa na maji mwilini.
Mlipuko wa ugongwa wa kipindupindu umeziathiri nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Ghana, Ivory Coast, NIgeria, Sudan na Togo.