Namna Ghaza inavyowabebesha jinamizi la kiafya wanajeshi wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130842-namna_ghaza_inavyowabebesha_jinamizi_la_kiafya_wanajeshi_wa_israel
Makumi ya wanajeshi wa utawala wa wa Kizayuni wa Israel waliovamia Ghaza wameambukizwa magonjwa ya ngozi ya kuambukiza.
(last modified 2025-09-16T02:17:48+00:00 )
Sep 16, 2025 02:17 UTC
  • Namna Ghaza inavyowabebesha jinamizi la kiafya wanajeshi wa Israel

Makumi ya wanajeshi wa utawala wa wa Kizayuni wa Israel waliovamia Ghaza wameambukizwa magonjwa ya ngozi ya kuambukiza.

Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeripoti kuenea magonjwa "hatari" ya ngozi miongoni mwa wanajeshi wa Israel walioko Ghaza na kuandika: "Sehemu nyingi za eneo la Ghaza zimechafuliwa na ni maeneo hatarishi kutokana na uhaba wa maji, ukosefu wa huduma za kimsingi za afya na kuhama mamia ya maelfu ya Wapalestina. Nyumba zilizoharibiwa zimekuwa makazi ya wanyama pori na wanyama hatari wanaorandaranda ovyo kila mahali."

Kwa hakika kuchafuliwa mazingira na kusababishwa maafa ya kiafya kwa wananchi wa Ghaza yameathiri si tu maisha ya Wapalestina, lakini pia maisha ya wanajeshi vamizi wa Israel.

Hali mbaya na chafu ya kimazingira inayotokana na vitendo vya kikatili na kiharibifu vya wanajeshi wa Israel kwenye miundombinu ya Ghaza imepelekea si tu Wapalestina wa Ghaza kuishi katika hali mbaya ya kiafya, lakini pia wanajeshi wa Israel sasa wamekumbwa na jinamizi la magonjwa ya ngozi. 

Kiujumla ni kwamba, kukithiri matatizo ya kiafya huko Ghaza kumesababisha wanajeshi wengi wa Israel kukumbwa na magonjwa kama vile kuwashwa sana kwenye ngozi na vipele vinavyotokana na kuumwa na kunguni hasa nyakati za usiku. Matatizo hayo yanaenea kwa kasi kati ya wanajeshi wa Israel. Mengi ya magonjwa hayo huambukizwa kwa urahisi kupitia vifaa vya kijeshi kama vile sare za vita, mifuko ya kulalia na vitu vingine.

Mgogoro huu wa kiafya ambao ni matokeo ya moja kwa moja ya uharibifu wa miundombinu ya afya na matibabu huko Ghaza, si tu umeathiri moyo wa kuendelea na vita wanajeshi wa Israel lakini pia umepunguza uwezo wa kiutendaji wa jeshi la Kizayuni.

Wanajeshi vamizi wa Israel wanakumbwa na majinamizi mengi Ghaza

 

Gazeti la Yedioth Ahronoth limemnukuu afisa wa akiba wa jeshi la Israel akisema: Wanajeshi wa Israel wamekuwa wakiteseka kimya kimya kwa wiki kadhaa sasa. Kulala chini katika maeneo yaliyochafuliwa ndio sababu kuu ya magonjwa haya. Hata wale wanaolala kwenye vitanda hawako salama kutokana na kutafunwa na wadudu, kwani kunguni huambukizwa kupitia sare za kijeshi na mashuka ya kulalia, na hii ni katika hali ambayo mahitaji ya kimsingi kama vile bafu hayapatikani. Maeneo makubwa ya Ghaza yamekuwa machafu na hatari kwa sababu ya uhaba wa maji, ukosefu wa mahitaji ya kimsingi kama vyoo, na mamia ya maelfu ya Wapalestina kuhama makazi yao.

Kuendelea kuripuliwa kwa mabomu Ghaza na kuendelea utawala wa Kizayuni kuharibuu miundombinu ya afya na matibabu kumewaweka Wapalestina kwenye wakati mgumu sana. Hospitali na vituo vya afya ambavyo huko nyuma vilikuwa vinawasaidia sana watu, hivi sasa vimekuwa magofu. Vifaa vingi vya matibabu haviko katika hali inayotakiwa na madaktari na dawa hazipatikani. Uharibifu wa miundombinu kama vile maji safi ya kunywa, hayako tena.

Takwimu zinaonyesha kwamba licha ya kuwa familia nyingi za Wapalestina zimelazimika kutafuta matibabu katika maeneo mengine, lakini haiwezekani kukwepa mgogoro huu, na hali inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Yote hayo yamefanywa na wanajeshi makatili wa Israel kwa kudhani kuwa watakaoteseka ni Wapalestina tu lakini sasa na wao wamekumbwa na jinamizi la mgogoro wa kiafya kiasi kwamba majeraha ya miilini mwao yamedhoofisha ari ya wanajeshi wa Israel huko Ghaza. Mara nyingi, wanajeshi wa Israel wanashindwa kuendelea kufanya jinai huko Ghaza si kwa kupenda, bali kutokana na hali duni ya usafi na magonjwa ya ngozi yanayowasambaratisha wanajeshi hao makatili. Hata kumekuwa na ripoti za baadhi ya wanajeshi wa Israel kukimbia maeneo ya vita.

Vyombo vya habari vya Kizayuni pia viliripoti kuwa wanajeshi wa Israel wameugua magonjwa ya akili na mwelekeo wa kutaka kujiua kutokana na vita vya Ghaza. Zaidi ya wanajeshi elfu mbili katika vita vya ardhini dhidi ya Ghaza wamelazimika kuwauona madaktari wa magonjwa ya akili kutokana na matatizo ya kiakili na kisaikolojia.

Idara ya kusimamia masuala ya jeshi la Israel imelazimika kuunda timu ya wauguzi na madaktari wa akili ili kuwasaidia wanajeshi wanaojiua na wanaoteseka kutokana na magonjwa ya wasiwasi na kiakili kutokana na vita huko Gaza.

Kwa hakika kuenea maradhi hayo kwa upande mmoja kunaashiria hali mbaya na ya kikatili ambayo jeshi la Israel limewasababishia Wapalestina wanaoishi Ghaza, na kwa upande mwingine ni onyo kwamba hata wale wanaochochea vita hawawezi kuwa salama kutokana na matokeo mabaya ya vita.

Mgogoro wa kiafya huko Ghaza si tu ni maafa ya kibinadamu kwa Wapalestina, lakini pia unaonyesha kuwa ukatili na ghasia zozote katika vita zina madhara makubwa kwa pande zote, hata ule unaochochea na kusababisha uharibifu huo.