Jul 31, 2024 02:40 UTC
  • UN: Wapalestina Gaza wanahitaji chanjo haraka ili kuzuia polio

Katika jitihada za kuzuia janga la ugonjwa wa polio huko Gaza, mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa jana Jumanne yalikariri wito wa kufanyika jitihada za kimataifa za kuutaka utawala wa Israel usitishe vita ili kuruhusu kampeni kubwa ya utoaji chanjo kuanza.

Takriban miezi 10 ya vita na mashambulizi makali ya utawala katili Israel imesambaratisha huduma ya afya katika Ukanda wa Gaza na kuvuruga mzunguko wa kawaida wa utoaji chanjo kwa watoto, na kuwaacha wakiwa kwenye hatari ya kupata magonjwa mbalimbali yanayoweza kuzuilika ukiwemo ugonjwa hatari wa kupooza, polio. Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kuwepo kwa wagonjwa wa polio baada ya kufanyiwa uchunguzi sampuli kadhaa za maji taka zilizochukuliwa kutoka Gaza.

Gaza

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva huko Uswisi, msemaji wa WHO, Christian Lindmeier alisema kuwa usitishaji mapigano utakuwa suluhisho "bora zaidi", kabla ya kutoa wito angalau kwa barabara za eneo hilo kuwekwa wazi na kusaidia upatikanaji salama wa matibabu na vifaa vingine vya msaada viweze kupita.

Tangu Israel ianzishe mauaji ya kimbari ya Gaza mwezi Oktoba mwaka jana, imewauwa takriban watu 40,000 wa Palestina, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na vijana. Wapalestina wengine zaidi ya 90,000 wamejeruhiwa mbali na kusambaratika kikamilifu mfumo wa afya eneo hilo.

Tags