Kinshasa na M23 waanza tena mazungumzo Qatar katika juhudi za kutekeleza makubaliano ya kusitisha vita
Duru mpya ya mazungumzo kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 inaendelea katika mji mkuu wa Qatar, Doha. Pande hizo mbili zinatazamia kufikia makubaliano juu ya namna ya kutekeleza mapatano waliyosaini mwezi uliopita kwa upatanishi wa Qatar.
Hata hivyo mapigano yameripotiwa kujiri katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo licha ya kufikiwa mapatano hayo.
Duru hii mpya ya mazungumzo itajikita katika rasimu iliyopendekezwa na Qatar kwa ajili ya mchakato wa amani wa awamu tatu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar amesema kuwa majadiliano yanayoendelea sasa yanajumuisha mipango ya kubuni mfumo wa kusimamia mapatano ya kusimamisha vita pamoja na kubadilishana mateka.
Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji jana Jumanne aliwaambia waandishi wa habari kuwa Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari ameeleza kutoridhishwa na rasimu iliyopendekezwa.
Serikali ya Kongo na waasi wa M23 kila upande unautuhumu mwenzake kuwa amekiuka makubaliano ya kusitisha vita.