Maandamano yashadidi nchini Ethiopia, Umoja wa Mataifa wataka kutumwa waangalizi wa kimataifa
Maandamano dhidi ya serikali ya Ethiopia yanazidi kushadidi huku serikali ya nchi hiyo ikitumia vyombo vya usalama kuwakandamiza waandamanaji.
Maandamano hayo ambayo kitovu chake ni katika miji ya Oromia na Amhara yanashadidi katika hali ambayo, idadi ya watu waliouawa na vikosi vya usalama katika kuyakandamiza maandamano hayo dhidi ya serikali imefikia mia moja.
Serikali ya Ethiopia imekuwa ikikabiliwa na upinzani mkali wa jamii za makabila mawili makubwa nchini humo ya Oromo na Amhara. Watu wa makabila hayo wamekuwa wakifanya maandamano kulalamikia siasa mbovu za serikali ya Addis Ababa.
Wakati Katika kukabiliana na uhamasishaji, serikali ya Ethiopia imeendelea kufunga mitandao yote ya kijamii nchini humo na kupiga marufuku maandamano ya aina yoyote.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kutumwa waangalizi nchini Ethiopia kutokana na kukithiri vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa na vikosi vya serikali ya Addis Ababa.
Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, umoja huo una wasiwasi mkubwa kutokana na hali inayotawala hivi sasa nchini Ethiopia.
Awali maandamano hayo ambayo yalianza kwa ajili ya kupinga uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kuyajumuisha baadhi ya maeneo ya mji wa Amhara na eneo la Tigray sasa yanaonekana kuchukua sura ya kisiasa.