Afrika Kusini imewahukumu raia 7 wa China miaka 20 jela kila mmoja kwa magendo ya binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130674-afrika_kusini_imewahukumu_raia_7_wa_china_miaka_20_jela_kila_mmoja_kwa_magendo_ya_binadamu
Mahakama moja mjini Johannesburg Afrika Kusini imewahukumu raia saba wa China kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kia mmoja baada ya kuwapata na hatia ya magendo ya binadamu. Raia hao wa China wamekutwa na hatia ya kuwasafirisha watu kutoka Malawi na kuwalazimisha kufanya kazi katika kiwanda kimoja nchini Afrika Kusini.
(last modified 2025-09-11T11:03:53+00:00 )
Sep 11, 2025 11:03 UTC
  • Afrika Kusini imewahukumu raia 7 wa China miaka 20 jela kila mmoja kwa magendo ya binadamu

Mahakama moja mjini Johannesburg Afrika Kusini imewahukumu raia saba wa China kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kia mmoja baada ya kuwapata na hatia ya magendo ya binadamu. Raia hao wa China wamekutwa na hatia ya kuwasafirisha watu kutoka Malawi na kuwalazimisha kufanya kazi katika kiwanda kimoja nchini Afrika Kusini.

Kundi hilo la Wachina saba lilipatikana na hatia Februari 25 mwaka huu ya kuwasafirisha bila vibali raia 91 wa Malawi kuanzia mwaka  2017 hadi 2019  ili kufanya kazi katika kiwanda cha vitambaa vya pamba huko Village Deep, eneo la viwanda kusini mwa mji wa Johannesburg.

Wachina hao walitiwa ngvuni Novemba 12 mwaka 2019 wakati polisi walipovamia kiwanda hicho na kuwakuta raia kadhaa wa Malawi wakiwa wanatumikishwa katika mazingira yasiyo ya kibinadamu huku walinzi wenye silaha wakidhibiti mienendo yao.

Rekodi za mahakama zimewataja Wachina hao waliohukumiwa jela kuwa ni Shu-Ueu Tsao mwenye miaka 42, Biao Ma miaka 50, Hui Cheni miaka 50, Qiuin Li miaka 56, Zhou Jiaquing miaka 46. zjunying Dai miaka 58 na Zhilian Zhang miaka 51. 

Mahakama ya  Kusini ya Gauteng nchini Afrika Kusini imewahukumu Wachina hao wote kifungo cha miaka 20 jelal kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya magendo ya  binadamu na kuvunja sheria za kazi na uhamiaji za nchi hiyo.

Waendesha mashtaka katika mahakama ya Gauteng walitaka raia hao wa China wahukumiwe kifungo cha maisha jela wakisema kuwa wahanga wa magendo ya binadamu walikuwa wakilazimishwa kufanya kazi katika zamu ya masaa 12 na kufanya kazi kwa siku saba zote za wiki bila ya kupatiwa mafunzo stahili na vifaa vya kudhamini usalama wao. 

Wamesema kuwa, raia wengi awali walikuwa wakifanya kazi katika viwanda vinavyomilikiwa na Wachina huko Malawi na waliajiriwa kwenda Afrika Kusini kwa visingizio mbalimbali.