Watu 100 wahofiwa kuaga dunia kwa kufukiwa mgodini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131326-watu_100_wahofiwa_kuaga_dunia_kwa_kufukiwa_mgodini_nigeria
Takribani watu 100 wanahofiwa kufariki dunia baada ya kufukiwa na vifusi vya mgodi wa dhahabu katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.
(last modified 2025-09-27T22:59:12+00:00 )
Sep 27, 2025 22:59 UTC
  • Watu 100 wahofiwa kuaga dunia kwa kufukiwa mgodini Nigeria

Takribani watu 100 wanahofiwa kufariki dunia baada ya kufukiwa na vifusi vya mgodi wa dhahabu katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, mgodi huo uliopo katika eneo la Kadauri, wilaya ya Maru, uliporomoka Alkhamisi wakati wachimbaji wa kawaida walipokuwa wakiendelea na kazi chini ya ardhi,

Ripoti zinasema, operesheni za uokoaji ziliendelea hadi siku Ijumaa. Sanusi Auwal, mkazi wa eneo hilo aliyehusika katika juhudi za uokoaji, alisema kwamba miili 13 tayari imetolewa kutoka kwenye mabaki ya mgodi, ikiwa ni pamoja na mwili wa binamu yake.

“Zaidi ya wachimbaji 100 walikuwepo chini wakati mgodi ulipoporomoka,” Auwal alisema kwa simu. “Tuna bahati tumeokolewa hai. Tulikuwa zaidi ya watu 100, sisi 15 tu ndio tuliookolewa,” alisema Isa Sani, ambaye kwa sasa anapatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyopata.

Muhammadu Isa wa chama cha wachimbaji wa jimbo la Zamfara alithibitisha kutokea tukio hilo, akiongeza kwamba, baadhi ya waokoaji walipata Dhoruba wakati wakijaribu kutoa wahanga wa tukio hilo.

Msemaji wa polisi yam ji wa Zamfara, Yazid Abubakar, hakutoa maelezo alipoombwa kwa simu na ujumbe wa maandishi kutoa maoni yake. Uchimbaji haramu ni wa kawaida Zamfara, ambapo makundi yenye silaha mara nyingi hushikilia usimamizi wa migodi ya dhahabu, hali inayochochea vurugu na ajali zinazosababisha vifo.