Iran yataka UN na nchi wanachama zikatae “ugaidi wa kiuchumi” wa Marekani
-
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi wanachama wa umoja huo kukataa kampeni mpya ya Marekani ya ugaidi wa kiuchumi dhidi ya Iran, akisema Washington inalenga kuzilazimisha nchi nyingine kuacha mahusiano halali ya kiuchumi na Tehran kwa kutumia vitisho vya vikwazo.
Katika barua aliyowaandikia Jumatano Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais wa Baraza la Usalama, pamoja na nchi wanachama wa UN, Araghchi amesema hatua zilizotangazwa hivi karibuni na Marekani chini ya kile kinachoitwa “Operesheni ya Kutengwa Kiuchumi” ni jaribio la kulazimisha sera za Marekani kwa mataifa yenye mamlaka kamili.
Araghchi ameutaka Umoja wa Mataifa kulaani hatua hizo, kujizuia kuzitambua au kuzitekeleza, na kuishinikiza Washington ikomeshe vitisho dhidi ya nchi zinazodumisha mahusiano ya kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa barua hiyo, lengo lililotangazwa la kampeni ya Marekani ni kukomesha mahusiano halali ya kiuchumi na Iran kwa kutishia nchi na taasisi mbalimbali kwa vikwazo vinavyojumuisha kuzuia kutumia mfumo wa kifedha wa Marekani.
Araghchi amesema hatua hizo ni sawa na juhudi za kutekeleza sheria za Marekani na malengo yake ya sera za kigeni nje ya mipaka yake, na kuzilazimisha serikali nyingine zibadilishe sera zao huru za kiuchumi.
Sehemu muhimu ya barua hiyo ilihusu athari za hatua za Marekani kwa raia wa Iran.
Araghchi ameikosoa Marekani kwa kuwalenga raia kwa makusudi.
Barua hiyo pia imebaini dhamira ya Iran ya kufuata njia za kisheria na kidiplomasia dhidi ya hatua za Marekani zinazokiuka sheria.
Aidha, barua hiyo imesema kuwa Marekani inabeba dhima kwa madhara yanayotokana na hatua zisizo halali zinazoilenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wakati huohuo, msemaji wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema Lango Bahari la Hormuz litaendelea kufungwa hadi pale Marekani itakapokomesha mzingiro wake dhidi ya Iran na ikubali masharti ya Iran kuhusu utekelezaji wa Hati ya Makubaliano (MoU) iliyofikiwa hivi karibuni.
Brigedia Jenerali Hossein Mohebbi alisema Jumatano kuwa njia hiyo ya kimkakati ya baharini iko chini ya udhibiti madhubuti wa Iran, na kwamba majeshi ya uadui yametimuliwa kutoka eneo hilo.
Amesema meli zote za kivita zimeondoka na kurudi umbali wa angalau kilomita 400 kutoka Lango Bahari la Hormuz, akiongeza kuwa, kwa mtazamo wa kijeshi na wa mamlaka ya kieneo, “hakuna chombo cha majini chenye uwezo wa kupita katika njia hii ya maji bila idhini na usimamizi wa Iran.”
Jenerali Mohebbi amesema kuwa iwapo Marekani itasitisha uingiliaji wake na kurejea katika mfumo wa mapatano yaliyotiwa saini mwezi Juni, Iran iko tayari kufungua tena Lango-Bahari hilo kwa mujibu wa makubaliano hayo.