Saudia yakimbilia Oman kuomba kusimamishwa vita Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141548-saudia_yakimbilia_oman_kuomba_kusimamishwa_vita_yemen
Baada ya kuanzisha vita vya miaka mingi kwa lengo la kuiteka Yemen, sasa hali ni ngumu sana kwa Saudi Arabia kiasi kwamba imefikia hatua ya kuomba msaada wa Oman iingilie kati ili kusimamisha mashambulizi ya Ansarullah na Jeshi la Yemen.
(last modified 2026-09-18T10:39:37+00:00 )
Sep 18, 2026 10:38 UTC
  • Saudia yakimbilia Oman kuomba kusimamishwa vita Yemen

Baada ya kuanzisha vita vya miaka mingi kwa lengo la kuiteka Yemen, sasa hali ni ngumu sana kwa Saudi Arabia kiasi kwamba imefikia hatua ya kuomba msaada wa Oman iingilie kati ili kusimamisha mashambulizi ya Ansarullah na Jeshi la Yemen.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, gazeti la Lebanon la "Al-Akhbar"* limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Saudi Arabia imekimbilia kwa Oman kuiomba iingilie kati na kuwezesha kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano na Yemen hata kwa kuanzia na makubaliano ya wiki mbili; kipindi ambacho mahitaji yote ya kibinadamu yatafanyiwa kazi.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Saudi Arabia imesema kuwa makubaliano ya mwisho kuhusu mahitaji ya kibinadamu yatatangazwa baada ya wiki moja. Hata hivyo, Yemen inasisitiza kuwa mahitaji yake yote lazima yatimizwe na kwamba wigo wa makubaliano hayo haupaswi kuishia kwenye maombi hayo mahususi pekee.

Kwa upande wake Shirika la Habari la Associated Press (AP) limeripoti leo kuwa Saudia imeomba msaada kwa washirika wake kutokana na kupungukiwa na silaha za mifumo ya kujilinda na mashambulizi ya anga tena wakati huu ikiwa iko katikati ya vita na Yemen.

Kwa mujibu wa shirika hilo la habari la Marekani, Saudi Arabia imekimbilia kwa "washirika wake wa kikanda na wa nchi za Magharibi" kuomba msaada wa silaha.

Shirika hilo limewanukuu maafisa wawili wa nchi za ukanda huu wakithibitisha kuwa akiba ya Saudi Arabia ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya anga inakaribia kwisha huku mapigano kati yake na jeshi la Yemen yakiendelea na hakuna dalili yataisha lini.

Maafisa hao wamesema kuwa Saudi Arabia imeziomba Ufaransa, Uingereza, Pakistan na Misri kupeleka vikosi vya ulinzi wa anga na zana za kivita kuisaidia kwenye vita vyake na Yemen na kukabiliana na makombora na droni (ndege zisizo na rubani) za Yemen.