Al-Hajj Ali-Akbari: Hatutofanya mazungumzo hadi masharti ya Kiongozi Muadhamu yatimizwe
Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran amesema kuwa: "Hakutakuwa na mazungumzo yoyote hadi pale masharti yote yaliyowekwa na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu yatakapotimizwa. Kwa taufiki ya Allah, tutaendelea kuwa macho mbele ya njama hatari za adui."
Hujjatul Islamu wal Muslimin Alhajj Ali-Akbari, amesema hayo kwenye khutba za Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa Tehran na huku akigusia umuhimu wa familia na uhusiano wake na maisha ya kijamii ya mwanadamu amebainisha kuwa, madola ya kibeberu ya Magharibi yanaeneza ufuska ili kuyadhibiti mataifa ya dunia.
Amesema, utamaduni wa kisasa wa Magharibi wa kueneza ufuska, ukosefu wa staha na mmomonyoko wa maadili, umeleta uharibifu mkubwa kwa familia, madhara ambayo jamii za Magharibi zenyewe hivi sasa zimeemewa na hazijui cha kufanya.
Amesema, upuuzi na ujinga unaonezwa hivi sasa wa kuinua juu bendera ya ukosefu wa aibu, ukosefu wa staha na uhuru uliopitiliza wa kimapenzi; uliopelekea kuvuka mipaka ya amri zote za Mwenyezi Mungu na kukanyaga mipaka ya kimaadili; kwa kutanguliza anasa za kijinga na kipuuzi; umetenda moja ya jinai na uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya binadamu yaani kusambaratisha muundo wa familia.
Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran pia amesema kwenye khutba zake hizo mbili kwamba: "Walioanzisha utamaduni huu walitumia sayansi, teknolojia, sanaa na hoja za kifalsafa na nguvu kubwa, kueneza utamaduni huu uliopotoka hadi katika jamii nyingine; kupitia mashambulizi makubwa ya kiutamaduni; na kwa kweli wameleta madhara makubwa kwa maisha ya jamii nyingi.
Katika sehemu nyingine ya khutba zake, Al Hajj Ali-Akbari amesema: "Jamii isiyo na mifumo imara ya kifamilia huzaa watu wasio na uhusiano wa kifamilia. Huzalisha pia watu wanaoishi bila ya mfungamano wala misingi imara. Huzaa watu ambao hawana hisia ya utambulisho wa kitaifa. Inapofikia hivyo, huwa ni rahisi kwa madola ya kibeberu kuitawala jamii hiyo na kupora rasilimali pamoja na utajiri wake wa kitaifa."