Kuendelea mashambulio dhidi ya vinu vya kusafisha mafuta Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13135-kuendelea_mashambulio_dhidi_ya_vinu_vya_kusafisha_mafuta_nigeria
Kundi jipya la wabeba silaha lililoundwa katika eneo la Niger Delta nchini Nigeria limeonya kuwa litafanya mashambulio zaidi ya ilivyokuwa hapo kabla dhidi ya vinu vya kusafisha mafuta vya makampuni ya kigeni yaliyoko katika eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 12, 2016 11:01 UTC
  • Kuendelea mashambulio dhidi ya vinu vya kusafisha mafuta Nigeria

Kundi jipya la wabeba silaha lililoundwa katika eneo la Niger Delta nchini Nigeria limeonya kuwa litafanya mashambulio zaidi ya ilivyokuwa hapo kabla dhidi ya vinu vya kusafisha mafuta vya makampuni ya kigeni yaliyoko katika eneo hilo.

Kundi la wanamgambo linalojiita Niger Delta Greenland Justice Mandate ambalo limetangaza uwepo wake hivi karibuni limeonya kuwa kuanzia sasa hakuna kinu chochote cha mafuta cha makampuni ya kigeni kitakachobaki salama katika eneo la Niger Delta.

Kundi hilo jipya limetangaza kuwa ndilo lililohusika na shambulio kali la jana Alkhamisi lililolenga kinu cha mafuta cha kampuni ya mafuta ya Shorelines na kutishia kwamba itaendelea kufanya mashambulio makali zaidi ya aina hiyo.

Niger Delta Greenland Justice Mandate limeongeza kuwa litaendelea kushambulia na kuripua vinu vya kusafisha mafuta sambamba na mashambulio yanayofanywa na kundi la Niger Delta Avengers.

Kundi la wanamgambo la Niger Delta Avengers

Uwepo wa kundi hilo jipya la wanamgambo ulitangazwa siku mbili zilizopita na mtu aliyejitambulisha kuwa msemaji wake aliyejiita Jenerali Aldo Agbalaja. 

Kundi la Niger Delta Greenland Justice Mandate limeyataka makampuni yote yanayochimba mafuta nchini Nigeria yaondoe wafanyakazi wao katika eneo la Niger Delta.

Itakumbukwa kuwa katika miezi michache iliyopita, makundi ya wanamgambo yameshambulia mara kadhaa mitambo na vinu vya kusafisha mafuta katika eneo la Delta huko kusini mwa Nigeria, mashambulio ambayo yamesababisha hasara kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo.

Vinu na mabomba ya mafuta yaripuliwa katika eneo la Niger Delta

Nigeria ni moja ya wazalishaji wakubwa wa mafuta barani Afrika na sehemu kubwa ya uchumi wake unategemea pato linalotokana na mauzo ya mafuta. Kwa sababu hiyo sambamba na kupungua bei ya mafuta katika soko la dunia, mashambulio hayo ya mtawalia yamesababisha kupungua uzalishaji wa mafuta wa nchi hiyo na kuathiri vibaya uchumi wake.

Takwimu zinaonyesha kuwa pato la fedha linalotokana na uuzaji mafuta linadhamini zaidi ya asilimia 95 ya pato lote la uuzaji bidhaa nje na kuchangia asilimia 80 ya mapato ya serikali ya Abuja.

Msemaji wa Shirika la Taifa la Mafuta la Nigeria Garba Mohammed alitangaza hapo kabla kuwa uzalishaji wa mafuta ghafi umepungua kutoka mapipa milioni mbili na laki mbili hadi milioni moja na laki sita kwa siku.

Huko nyuma ni kundi la waasi la Niger Delta tu ndilo lililokuwa likifanya mashambulio katika eneo la Niger Delta, lakini kutokana na kujitokeza makundi mengine likiwemo kundi jipya la Niger Delta Greenland Justice Mandate, inaonesha kuwa hali ya mambo katika eneo hilo itakuwa ngumu na tata zaidi.

Kwa mujibu wa wataalamu, lengo la kufanywa mashambulio hayo ni kuyatimua makampuni ya kigeni yanayofanya shughuli zao katika eneo la Niger Delta. Waasi wa Niger Delta wanaitakidi kuwa makampuni hayo yanapora utajiri wa taifa wa nchi yao.

Makampuni kadhaa ya mafuta ya kigeni yanafanya shughuli zao Niger Delta

Aidha wanataka eneo hilo litengewe fungu kubwa zaidi katika pato linalotokana na mauzo ya mafuta.

Kutokana na kushtadi mashambulio, viongozi wa serikali ya Nigeria wametoa wito mara kadhaa wa kusitishwa mashambulio na kurejeshwa usalama katika eneo la Niger Delta. Katika kile ilichoeleza kuwa nia ya kutafuta ufumbuzi wa kukomesha mapigano na machafuko katika eneo hilo, serikali ya Abuja ilitangaza kuwa iko tayari kufanya mazungumzo na wawakilishi wa kundi la waasi wa Niger Delta, lakini kundi hilo limekataa kufanya mazungumzo ya aina yoyote na serikali.

Rais Buhari amewahi kutangaza kuwa yuko tayari kuzungumza na waasi

Kufuatia hali hiyo serikali ya Abuja iliamua kutuma kikosi maalumu cha jeshi kwa lengo la kupambana na kundi hilo na kulinda usalama wa vinu vya mafuta katika eneo hilo. Hata hivyohatua hiyo imewatia wasiwasi wakaazi wa Niger Delta.

Amani katika eneo hilo imevurugika katika hali ambayo vita vikali vya kupambana na kundi la Boko Haram ni miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele na serikali ya Nigeria. Sambamba na kundi hilo la kigaidi na kitakfiri kuteketeza maeneo mengi ya miji ya nchi hiyo, njaa nayo inatishia idadi kubwa ya raia waliolazimika kuwa wakimbizi kwa sababu ya kukimbilia maeneo ya usalama.

Kundi la kigaidi la Boko Haram

Katika hali kama hii, inavyoonekana, kuandaa mazingira ya mazungumzo na kufikia kwenye njia ya ufumbuzi wa pamoja kunaweza kuwa ndio hatua mwafaka ya kuepusha kuzuka mgogoro mwengine mkubwa nchini Nigeria na katika eneo zima la magharibi mwa Afrika.../