Mripuko wa boti magharibi mwa Libya waua watu kadhaa
Watu wasiopungua watatu wamethibitishwa kuuawa katika mripuko wa boti uliotokea kwenye pwani ya Zawiya, karibu kilomita 60 magharibi mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Taarifa hiyo imetolewa na gazeti la Al-Marsad la Libya na kuongeza kuwa, mbali na vijana watatu wa Libya waliopoteza maisha kwenye mripuko huo na ambao wametambuliwa kwa majina ya Mohamed Ben Shtwan, Anwar Al-Majdoub na Nasser Sultan, kuna majeruhi wengine kadhaa wa tukio hilo ambao hadi wakati wa kuripotiwa habari hii walikuwa bado hawajulikana majina na utambulisho wao ukiwemo uraia wao.
Ripoti hiyo haikubainisha muda hasa wa tukio hilo na kilichosababisha boti hiyo kuripuka. Gazeti hilo limeandika: "Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusiana na tukio hilo."
Libya imekuwa kituo kikubwa cha wahamiaji haramu wanaojaribu kufika barani Ulaya kwa ndoto za maisha bora. Wimbi hilo limekuwa kubwa tangu wakati wa uasi wa wananchi wa mwaka 2011 yaliyoungwa mkono na jeshi la nchi za Magharibi NATO. Kampeni hiyo ndiyo iliyomuondoa madarakani Muammar Gaddafi. Magenge ya kigaidi na magendo mbalimbali yakiwemo magendo ya binadamu yamepata nguvu sana nchini Libya tangu wakati huo na suala ambalo linawatumbukiza wahamiaji kwenye hatari kubwa sana ikiwa ni pamoja na kupigwa mnada masokoni kama watumwa.
Hadi hivi sasa Libya imegawanyika na inaongozwa na serikali mbili na mabunge mawili tofauti, moja ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye makao yake makuu mjini Tripoli na nyingine ni ile inayotawala upande wa mashariki kwa kushirikiana na jeshi linaloongozwa na Generali Khalifa Haftar.