Deng Gai: Machar ndiye anayekwamisha mchakato wa amani S/Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13441-deng_gai_machar_ndiye_anayekwamisha_mchakato_wa_amani_s_kusini
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Taban Deng Gai amemlaumu mtangulizi wake katika kiti hicho Riek Machar aliyeutoroka mji wa Juba kuwa amevuruga mchakato wa amani na kukiuka makubaliano ya kusitisha machafuko ya miezi kadhaa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 17, 2016 09:25 UTC
  • Deng Gai: Machar ndiye anayekwamisha mchakato wa amani S/Kusini

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Taban Deng Gai amemlaumu mtangulizi wake katika kiti hicho Riek Machar aliyeutoroka mji wa Juba kuwa amevuruga mchakato wa amani na kukiuka makubaliano ya kusitisha machafuko ya miezi kadhaa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Deng Gai ameyasema hayo leo mjini Nairobi, siku moja baada ya kufanya mazungumzo ya faragha na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kuhusu mgogoro wa kisiasa na mapigano mapya nchini Sudan Kusini. Amesema kuwa, Machar alijaribu kuendesha serikali mbili mjini Juba kabla ya kutoroka baada ya kushadidi mapigano kati ya askari wanaomuunga mkono na wale watiifu kwa Rais Salva Kiir.

Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini

Kadhalika Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini amebainisha kuwa, vikosi vya askari watiifu kwa Machar na Kiir vinatazamiwa kuunganishwa na kuwa jeshi moja kufikia mwezi Mei mwaka ujao 2017.

Vilevile amekariri kuwa, yuko tayari kumuachia Machar wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais iwapo atarejea mjini Juba kuendelea na mchakato wa kurejesha amani ya kudumu.

Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kukataa azimio lililopasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutumwa askari 4,000 zaidi wa kigeni nchini humo.

Mapigano mapya nchini Sudan Kusini ambayo hadi sasa yamepelekea watu zaidi ya 300 kuuawa yanaendelea licha ya uwepo wa askari 12,000 wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa (UNMISS) katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.