Askari kadhaa wa Saudia wauawa katika matukio tofauti
Duru za habari nchini Saudia zimeripoti kuuawa kwa kupigwa risasi afisa mmoja wa polisi, mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia imetangaza kuwa, watu wanne waliokuwa wamejifunika nyuso zao walimshambulia afisa huyo wa polisi eneo la Qatif, mashariki mwa Saudia na kumuua. Inafaa kuashiria kwamba, maeneo ya mashariki mwa Saudia yamekuwa yakishuhudia hali ya mchafukoge inayotokana na upinzani wa wakazi wa maeneo hayo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Aal-Saud.
Wakati huo huo, kanali ya televisheni ya al-Masirah ya Yemen imeripoti kwamba, kikosi cha mizinga cha jeshi la Yemen kwa kushirikiana na harakati za wananchi nchini humo, kimeshambulia kwa makombora eneo la askari vamizi wa Saudia katika kambi ya kijeshi ya Al-Sudais iliyopo mji wa Najran, kusini mwa Saudia, ambapo askari wengi wa nchi hiyo wameangamizwa. Shambulizi hilo limetekelezwa ikiwa ni katika kujibu jinai za Saudia nchini Yemen.
Hii ni katika hali ambayo televisheni ya al-Mayadin ya nchini Lebanon pia imeripoti kuangamizwa askari wengine watatu wa Saudia kwa kupigwa risasi na wapiganaji wa Yemen, katika eneo la Jizan, kusini mwa Saudia.