Jeshi la Somalia laangamiza makumi ya magaidi wa al-Shabaab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135012-jeshi_la_somalia_laangamiza_makumi_ya_magaidi_wa_al_shabaab
Makumi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye misimamo ya kufurutu ada , wameangamizwa katika operesheni ya wanajeshi wa Somalia.
(last modified 2026-01-02T07:57:23+00:00 )
Jan 02, 2026 02:47 UTC
  • Jeshi la Somalia laangamiza makumi ya magaidi wa al-Shabaab

Makumi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye misimamo ya kufurutu ada , wameangamizwa katika operesheni ya wanajeshi wa Somalia.

Wizara ya Ulinzi ya Somalia ilisema katika taarifa yake jana Alkhamisi kwamba, wanajeshi wa Somalia wamewaangamiza wanamgambo 29 wa al-Shabaab katika mji wa Jabad Godane kusini mashariki mwa Somalia, kwa ushirikiano na washirika wa kimataifa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, wanajeshi wa Somalia walijibu mapigo na kuwashambulia magaidi hao, baada ya kushambulia kambi ya jeshi katika mji huo wa kusini mashariki, ambapo wengine kadhaa walifurushwa na baadhi wakakimbilia msituni.

Jeshi la Somalia likishirikiana na askari wa kieneo na kimataifa, katika miezi ya karibuni limefanikiwa kuukomboa miji kadhaa ya kistrataji katika maeneo ya kusini mwa Somalia, toka mikononi mwa al-Shabaab.

Hivi karibuni, wataalamu wa Umoja wa Mataifa walitahadharisha katika ripoti yao kwamba, kundi lenye misimamo mikali la al-Shabaab lingali ni tishio kubwa hivi sasa kwa amani na uthabiti huko Somalia na katika eneo zima la Pembe ya Afrika ikiwa ni pamoja na katika nchi jirani ya Kenya.

Mwishoni mwa mwaka uliomalizika wa 2025, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura na kurefusha muda wa kuhudumu kikosi cha askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AU) huko Somalia hadi Disemba 31, 2026.

Tangu mwaka 2007, kundi hilo kigaidi lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.