Somalia yapokezwa uenyekiti wa kiduru wa Baraza la Usalama la UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135052-somalia_yapokezwa_uenyekiti_wa_kiduru_wa_baraza_la_usalama_la_un
Somalia jana Ijumaa ilichukua urais wa zamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwezi huu wa Januari, ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kushikilia wadhifa huo tangu ilipohudumu mara ya mwisho katika baraza hilo mwaka 1971-72.
(last modified 2026-01-03T06:03:34+00:00 )
Jan 03, 2026 06:03 UTC
  • Somalia yapokezwa uenyekiti wa kiduru wa Baraza la Usalama la UN

Somalia jana Ijumaa ilichukua urais wa zamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwezi huu wa Januari, ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kushikilia wadhifa huo tangu ilipohudumu mara ya mwisho katika baraza hilo mwaka 1971-72.

Akielezea tuki hilo kuwa la kihistoria, Balozi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa, Abukar Dahir Osman amesema wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwamba, "Somalia imeguswa sana kupokezwa urais wa Baraza la Usalama kufuatia nchi yetu kurudi kwenye baraza hilo baada ya miaka 54, ikiwa ilihudumu kwa mara ya mwisho katika muhula wa 1971-72. Hii ni hatua muhimu kwa nchi yangu."

Osman amesema kuteuliwa Somalia katika baraza hilo kuchukua urais "kunaashiria kujitolea kwa Somalia katika kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi." Amebainisha kuwa, katika mwaka uliopita, Somalia ilijitahidi kuwa na jukumu athirifu ndani ya baraza hilo. Somalia, amesema, imelenga kuwa "sauti ya hoja, mjenzi wa daraja, na mtetezi wa kuheshimiwa sheria za kimataifa, kufuata Hati ya Umoja wa Mataifa, ulinzi wa raia, na utatuzi wa migogoro kwa amani."

"Tunapochukua urais mwezi huu, Somalia itashikilia kiwango cha juu zaidi cha diplomasia na ushirikiano wa pande nyingi," amesema, akiongeza kuwa urais wa Somalia utaweka kipaumbele "ufanisi, uwazi, ujumuishaji, na ufikiaji wa makubaliano." 

Haya yanajiri katika hali ambayo, maelfu ya wananchi wa Somalia wameendelea kumiminika mabarabarani katika miji mbali mbali ya nchi hiyo, kupinga na kulaani uamuzi wa utawala haramu wa Israel wa kulitambua eneo la Somaliland la kama taifa huru. Hali kadhalika utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kulaaniwa kote duniani kwa kulitambua eneo hilo lililotangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991.