Uganda yaamuru mashirika ya haki kusitisha shughuli zao
-
Rais Yoweri Museveni wa Uganda
Uganda imeamuru mashirika mawili ya haki kusitisha shughuli zao, siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu ambao Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imeutaja kuwa unafanyika katika mazingira ya ukandamizaji na vitisho.
Mashirika yaliyoathiriwa ni Chapter Four Uganda na Human Rights Network for Journalists–Uganda, HRNJ-U. Mashirika hayo yamelaani hatua hiyo, na kusema uamuzi huo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Pia yametoa madai ya kukamatwa kiholela na kuteswa kwa wafuasi wa upinzani pamoja na wanahabari.
Katika barua kwa Chapter Four na iliyooonekana na shirika la habari la Reuters, Ofisi ya Kitaifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali inayosimamiwa na serikali ya Uganda, imedai kuwa shirika hilo linajihusisha na shughuli "zinazohatarisha" usalama wa taifa, na hivyo limetakiwa kusitisha kazi zake mara moja.
Wananchi wa Uganda waliotimiza masharti ya kupiga kura kesho Alkhamisi wanatajiwa kuelekea katika masanduku ya kupigia kura.
Akiwa na umri wa miaka 81, Museveni anawania kuchaguliwa tena akibeba bendera ya chama tawala cha National Resistance Movement, NRM baada ya kuweko madarakani kwa karibu miaka 40.
Mwaka 2017, Bunge la Uganda liliondoa ukomo wa umri wa kikatiba wa kuwania urais, na hivyo kutoa mwanya kwa Museveni kugombea kwa muda wowote anaotaka.
Mshindani wake mkuu Bobi Wine amejenga matumaini ya mabadiliko nchini humo. Mwimbaji huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita wa urais mnamo 2021, kwa kupata 35% ya kura
Wine alidai ushindi wake uliibwa kupitia ujazo wa kura na makosa mengine. Hata hivyo tume ya uchaguzi wa Uganda ilikanusha madai hayo.