Kenya: Umaskini wasababisha zaidi ya wanafunzi laki 8 kukosa kuripoti shule
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135500-kenya_umaskini_wasababisha_zaidi_ya_wanafunzi_laki_8_kukosa_kuripoti_shule
Ripoti kutoka Kenya zinasema umaskini pamoja na hatua ya serikali kudhibiti uteuzi wa shule, umeibuka kuwa sababu kuu inayofanya zaidi ya wanafunzi 800,000 wa Gredi ya 10 kushindwa kuripoti katika shule walizoteuliwa.
(last modified 2026-01-15T03:31:40+00:00 )
Jan 15, 2026 03:31 UTC
  • Wanafunzi laki 8 wakosa kwenda shule sababu ya umaskini
    Wanafunzi laki 8 wakosa kwenda shule sababu ya umaskini

Ripoti kutoka Kenya zinasema umaskini pamoja na hatua ya serikali kudhibiti uteuzi wa shule, umeibuka kuwa sababu kuu inayofanya zaidi ya wanafunzi 800,000 wa Gredi ya 10 kushindwa kuripoti katika shule walizoteuliwa.

Hali hiyo imesababisha msongo wa mawazo kwa wanafunzi na wazazi, huku baadhi ya watoto wakipatwa na huzuni kubwa kwa kushindwa kujiunga na shule walizoota.

Ripoti zinasema, baadhi ya shule zimeripoti kupokea chini ya wanafunzi 50 kati ya zaidi ya 500 waliotarajiwa.

Baadhi ya wanafunzi pia wanatafuta uhamisho baada ya kupelekwa shule zilizo mbali na nyumbani kwao au zisizoendana na matarajio yao ya taaluma.

Katika Kaunti ya Murang’a, Jacinta Njiru, mama mlezi anayejipa riziki kama mama-fua mjini Maragua, anasema hata akipewa miaka 10 ya kuweka akiba, hawezi kumudu karo ya Shilingi elfu 55, kwa mwanawe aliyeteuliwa kujiunga na Shule ya Upili ya Njiiri.

“Hiyo ni karo ya mwaka mmoja pekee. Pia ninatakiwa kununua mahitaji binafsi ya shule yanayozidi Shelfu 25,000,” alisema mama huyo kwa masikitiko.

Wadau sasa wanaitaka serikali ya Kenya kuongeza muda wa kuripoti, kuharakisha utoaji wa ufadhilina kuweka mikakati mahsusi ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayebaki nyuma kwa sababu ya umaskini.