Kenya yasaini makubaliano ya awali ya biashara na China
-
Kenya yasaini makubaliano ya awali ya biashara na China
Kenya imesaini makubaliano ya awali ya biashara na China ambayo yanaipa 98% ya mauzo yake ya nje ufikiaji usiotozwa ushuru katika soko kubwa la China. Hayo yameelezwa na serikali ya Nairobi huku makubaliano kamili na ya mwisho yakiendelea.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki imeimarisha uhusiano wake na China, huku Rais William Ruto akifanya ziara ya kiserikali Beijing mwaka jana, ambapo mikataba kadhaa ya ufadhili na ushirikiano ilisainiwa.
"Tumeanzisha mazungumzo na China ili kujadili makubaliano ya biashara ya pande mbili," wizara ya biashara ya Kenya imesema katika taarifa, ikifichua mazungumzo hayo kwa mara ya kwanza. "Mazungumzo haya yamepelekea kusainiwa makubaliano ya awali."
Makubaliano haya yanatokana na uamuzi wa Beijing wa kuondoa ushuru wote unaotumika kwa mataifa 53 ya Afrika ambayo inadumisha uhusiano wa kidiplomasia nayo, wachambuzi wamesema. Uamuzi huu ulitangazwa mwezi Juni mwaka uliyopita, kufuatia kampeni ya ushuru wa kimataifa iliyozinduliwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
"Ili tangazo hili lizingatie sheria za WTO, nchi zenye kipato cha kati kama Kenya lazima zifikie mikataba ya biashara ya pande mbili na China," amesema Hannah Ryder, mwanzilishi wa Development Reimagined, kampuni ya ushauri iliyobobea kuhusu Afrika.
Mikataba ya pande mbili hatimaye itakuwa ya pande zote mbili, amesema, lakini nchi za Afrika zitakuwa na muda wa kukuza uchumi wao ili kushindana na viwanda vikubwa ya China.
Kenya, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki, ilikuwa na nakisi ya biashara ya shilingi bilioni 549.82 (dola bilioni 4.27) na Beijing mwaka wa 2024, ikiwa imesafirisha bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 26.32 pekee kwenda China na kuingiza thamani ya shilingi bilioni 576.14.