Somalia yamteua mkuu mpya wa jeshi kuchukua nafasi ya Jenerali Rage
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136046-somalia_yamteua_mkuu_mpya_wa_jeshi_kuchukua_nafasi_ya_jenerali_rage
Baraza la Mawaziri la Somalia limemteua Brigedia Jenerali Ibrahim Mohamed Mohamud kuwa Kamanda mpya wa Jeshi la Taifa la Somalia (SNA). Hii ni kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia iliyosomwa na msemaji wa serikali, Abdinasir Ahmed Bashir.
(last modified 2026-01-30T02:49:22+00:00 )
Jan 30, 2026 02:49 UTC
  • Somalia yamteua mkuu mpya wa jeshi kuchukua nafasi ya Jenerali Rage

Baraza la Mawaziri la Somalia limemteua Brigedia Jenerali Ibrahim Mohamed Mohamud kuwa Kamanda mpya wa Jeshi la Taifa la Somalia (SNA). Hii ni kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia iliyosomwa na msemaji wa serikali, Abdinasir Ahmed Bashir.

Uteuzi huo umefanywa baada ya kutimuliwa Jenerali Odowa Yusuf Rage. Ibrahim Mohamed Mohamud alizaliwa mwaka 1995 na kuhitimu katika  Chuo cha Kijeshi cha Ankara nchini Uturuki katika Kitivo cha Utawala wa Umma kwa miaka mitano, ​​ambapo alisoma kuanzia mwaka 2013 hadi 2017. 

Brigedia Jenerali Ibrahim Mohamed Mahmud ni afisa mkuu wa kijeshi aliyehudumu kwa miaka 18 nchini Somalia na ana elimu ya chuo kikuu katika ngazi ya uzamili.

Kabla ya kupandishwa cheo, aliwahi kuwa Kamanda wa Kamandi ya Usaidizi wa Jeshi la Taifa la Somalia; nafasi ambayo aliichukua mwezi Juni 2024 kufuatia Amri ya Rais  Hassan Sheikh Mohamud kutokana na pendekezo la Waziri wa Ulinzi.

Kuteuliwa kwa Ibrahim Mohamed Mahamud ni sehemu ya mpango mpana zaidi wa kuunda upya na kuimarisha uwezo wa kiutendaji wa Jeshi la Taifa la Somalia, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa rasmi kwa Kamandi Kuu ya Usaidizi.

Mabadiliko ya uongozi katika Jeshi la Taifa la Somalia yanakuja wakati ambapo nchi hiyyo ikifanya jitihada za kuimarisha mafanikio katika uwanja wa vita ikiashiria mwelekeo mpya katika kuvipa vikosi vya jeshi utaalamu na kuhakikisha utayarifu endelevu wa operesheni za kurejesha usalama nchini humo.

Somalia imekuwa katika machafuko ya muda mrefu ikisumbuliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya wapiganaji wa kundi la al Shabab.