Serikali ya Somalia imechukua hatua gani katika kukabiliana na kujitenga kwa Somaliland?
Kufuatia kuongezeka harakati za watu wanaotaka kujitenga huko Somaliland baada ya kutambuliwa rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel, serikali ya Somalia imechukua hatua mpya za kukabiliana na harakati hizo katika eneo hilo.
Kuhusiana na hili, Rais Hassan Sheikh Mahmoud wa Somalia, katikati ya mvutano unaoendelea kuongezeka na eneo linalotaka kujitenga la Somaliland, alifika hivi karibuni katika mji wa Las Anod, mji mkuu wa jimbo la Sool kaskazini mashariki mwa Somalia linalodaiwa na mamlaka ya Somaliland, ambapo alikutana na kuzungumza na wajumbe wa ngazi ya juu kutoka Djibouti. Hii ni ziara ya kwanza ya rais wa Somalia katika mji wa Las Anod katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 iliyopita. Sheikh Mahmoud alisema katika hotuba yake mjini hapo: 'Leo ninasisitiza kwamba Jimbo la Kaskazini Mashariki ni sehemu rasmi ya serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Somalia. Jimbo la kaskazini mashariki mwa Somalia linajumuisha majimbo ya Sool na Sanag, ambayo yanadaiwa na eneo la Somaliland.
Pia, shirika la habari la taifa la Somalia "SONNA" lilitangaza kuwa mikataba yote iliyotiwa saini kati ya Somaliland na Umoja wa Falme za Kiarabu, ikiwa ni pamoja na mikataba ya usalama, ulinzi na bandari, imefutwa na serikali ya Mogadishu. Baraza la Mawaziri la Somalia lilitangaza kwamba kufutwa kwa mikataba yote na UAE kumetimia kufuatia ripoti na nyaraka za kuaminika kuhusu hatua za kiadui za Imarati dhidi ya Somalia, ambazo zinadhuru mamlaka, umoja wa ardhi na uhuru wa kisiasa wa Somalia. Serikali ya Somalia imesisitiza kuwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya kufanyika tathmini ya kina kuhusu hali ya hivi karibuni katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Somalia na China zimesisitiza katika taarifa ya pamoja kwamba Somaliland haiwezi kutenganishwa na Somaliland. Katika taarifa hiyo, China imetangaza kwamba inaunga mkono umoja wa ardhi ya Somalia na inaitambua Somaliland kama sehemu isiyoweza kutenganishwa na ardhi hiyo.
Eneo linalojitawala na linalotaka kujitenga la Somaliland lilijibu kauli ya serikali ya Somalia kwa kudai kwamba Mogadishu haina mamlaka yoyote ya kisheria juu ya bandari ya Berbera. Wizara ya Mambo ya Nje ya Somaliland imedai kuwa Somalia haikuwa sehemu ya makubaliano ya Somaliland wala mdhamini wa upande wowote katika mazungumzo hayo. Imeongeza: 'Mikataba yote iliyotiwa saini kati yetu na UAE ni ya kisheria na inatekelezeka kisheria.'
Msimamo huu wa Somaliland unamaanisha changamoto ya moja kwa moja kwa serikali kuu ya Somalia, ambayo inataka Somaliland irejee katika mamlaka yake. Bila shaka, uungaji mkono wa utawala wa Kizayuni pamoja na UAE kwa Somaliland umekuwa na nafasi muhimu katika kuchukuliwa msimamo huo mkali dhidi ya Somalia.
Hatua mpya za serikali ya Somalia katika kukabiliana na muelekeo wa kujitenga Somaliland zinafuatiliwa katika fremu ya malengo ya kisiasa, kiusalama na kiutawala. Somaliland ilijitangazia uhuru kwa upande mmoja tangu 1991, lakini hakuna nchi yoyote iliyoitambua rasmi. Hii ni katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni uliitambua Somaliland mwezi Disemba 2025 kutokana na malengo yake ya kujitanua. Katika miaka ya hivi karibuni na kutokana na kuongezeka kwa ushindani wa kikanda katika Pembe ya Afrika na kuingia katika eneo hilo wahusika wa kigeni, suala la Somaliland limekuwa nyeti zaidi kwa Mogadishu, ambapo serikali kuu imejaribu kuzuia mchakato wa kujitenga eneo hilo kupitia njia za kidiplomasia, kisheria na kiusalama.
Lengo la kwanza la Somalia ni kuleta utulivu katika ardhi yake na kuzuia kuthibiti mfano hatari katika eneo hilo. Serikali ya Mogadishu ina wasiwasi kwamba kutambuliwa rasmi au vinginevyo Somaliland na baadhi ya pande za kigeni, hasa katika muktadha wa makubaliano ya kiuchumi na kiusalama, kutadhoofisha msimamo wa serikali kuu na hivyo kuhimiza mikoa mingine kufuata mfano huo. Kwa hiyo, Somalia inajaribu kuzuia kutambuliwa rasmi Somaliland kwa kuongeza shughuli za kidiplomasia, kuonya kuhusu matokeo ya kisheria ya kujitenga na kupata uungaji mkono wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Lengo la pili ni kuzuia kupenya kwa madola ya kigeni katika eneo hilo ambalo lina umuhimu mkubwa wa kijiografia. Katika miaka ya hivi karibuni, eneo la Pembe ya Afrika limekuwa uwanja wa ushindani baina ya nchi mbalimbali, na Somalia ina wasi wasi kwamba maingiliano ya moja kwa moja ya baadhi ya serikali hususan utawala wa Kizayuni na Somaliland hasa katika maeneo ya bandari na kijeshi yataibua nyufa kubwa zaidi katika muundo wa nchi hiyo. Hatua mpya za Somalia kwa hakika ni jaribio la kudhibiti mchakato huo na kuzuia Somaliland kuwa ngome ya nchi za kigeni.
Lengo la tatu ni kuimarisha mshikamano wa ndani na kutuma ujumbe wa nguvu kwa makundi ya ndani. Serikali ya Somalia inajaribu kuonyesha kwamba ina uwezo wa kutumia mamlaka na kudhibiti migogoro ya ndani kwa kuchukua msimamo mkali na thabiti zaidi dhidi ya Somaliland. Hatua hizi pia ni sehemu ya juhudi pana za kukarabati serikali, kuimarisha taasisi za usalama na kuongeza imani ya umma katika muundo mkuu.
Inaonekana kuwa hatua mpya za Somalia zimechukuliwa si kwa ajili ya kuidhibiti Somaliland tu, bali ni sehemu ya mkakati mpana zaidi wa kulinda umoja wa kitaifa, kuzuia uingiliaji wa kigeni na kuimarisha serikali kuu katika mojawapo ya kanda nyeti zaidi za bara la Afrika.