Aug 27, 2016 07:37 UTC
  • Waislamu na Wakristo waanzisha kituo cha amani kati ya dini nchini Nigeria

Kwa mara ya kwanza Waislamu na Wakristo nchini Nigeria wameanzisha kituo amani kati ya wafuasi wa dini hizo nchini humo.

Kituo hicho cha kimataifa cha amani na mshikamano baina ya wafusi wa dini ya Uislamu na Ukristo, kimefunguliwa mjini Kaduna, katikati mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kituo hicho kitakuwa na jukumu la kueneza udugu kati ya wafuasi wa dini hizo nchini Nigeria kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kidini baina yao.

Viongozi wa Kikristo na Kiislamu wakiwa pamoja Nigeria

Wakati huo huo, baraza la makanisa duniani sanjari na kuashiria mapigano ya kidini ambayo yamekuwa yakitokea katika jimbo la Kaduna nchini humo, limesema kuwa kituo hicho kitageuka na kuwa mahala patakatifu kwa ajili ya kurejesha amani jimboni hapo. Kwa mujibu wa baraza hilo, mji wa Kaduna utakuwa kitovu cha amani na mshikamano baina ya wafuasi wa dini hizo mbili. Ni vyema kuashiria kuwa, zaidi ya watu 20 elfu wameuawa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita kutokana na mapigano yanayosababishwa na tofauti za kidini nchini humo.

Vijana Wakristo na Waislamu wakiwa pamoja wakionyesha ishara ya udugu

Hivi karibuni pia, Kituo cha Masuala ya Kijamii ya Waislamu na Kituo cha Kulinda Haki za Waislamu nchini Nigeria, kwa pamoja viliwatala Waislamu wote wa nchi hiyo kusimama kuwatetea Wakristo wanaokabiliwa na vitisho vya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram. Hatua hiyo ilikuja baada ya kinara wa kundi hilo, kutishia hivi karibuni kutekeleza mauaji na mashambulizi dhidi ya makanisa na wafuasi wa dini ya Kikristo nchini Nigeria.

Tags