Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaanza kutoa chanjo ya Ebola
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141026-jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_congo_yaanza_kutoa_chanjo_ya_ebola
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanza kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ebola ikiwa ni katika juhudi za kudhibiti mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa huo kuwahi kurekodiwa nchini humo.
(last modified 2026-08-28T09:56:07+00:00 )
Aug 28, 2026 09:55 UTC
  • Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaanza kutoa chanjo ya Ebola
    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaanza kutoa chanjo ya Ebola

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanza kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ebola ikiwa ni katika juhudi za kudhibiti mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa huo kuwahi kurekodiwa nchini humo.

Zoezi hilo limezinduliwa rasmi mjini Kisangani, makao makuu ya mkoa wa Tshopo, mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa zinasema kuwa, wahudumu wa afya na watu wengine walio mstari wa mbele katika kukabiliana na Ebola ni miongoni mwa watakaopewa chanjo kwanza.

Waziri wa Afya, Roger Kamba, amesema chanjo ya Ervebo itatolewa kwanza kwa wahudumu wa afya pamoja na watu waliowasiliana na wagonjwa.

Mlipuko huo umeenea katika mikoa sita, huku takwimu za serikali zikionyesha kuwa hadi Jumanne kulikuwa na visa 5,713 vilivyothibitishwa na vifo 2,744.

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema mlipuko huo bado haujadhibitiwa na huenda ukazidi ukubwa wa mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi uliotokea kati ya mwaka 2014 na 2016 na kusababisha zaidi ya vifo 11,000.

Hata hivyo, kuna changamoto kuhusu chanjo hiyo. Ebola inayosababisha mlipuko wa sasa ni aina ya Bundibugyo, wakati Ervebo imeidhinishwa dhidi ya aina nyingine, Zaire ebolavirus.

Kwa sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa mahsusi dhidi ya Ebola ya Bundibugyo. Chanjo ya Ervebo inatumika chini ya mpango wa matumizi ya huruma, huku wataalamu wakikusanya data ili kubaini iwapo inaweza kutoa kinga dhidi ya aina hiyo ya virusi.

Hayo yanajiri siku moja tuu baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuthibitisha kumalizika mlipuko wa Ebola nchini Uganda.

Mwezi uliopita Uganda ilitangaza rasmi kuwa haina tena maambukizi ya virusi hivyo siku 42 baada ya kuthibitishwa kuruhusiwa kutoka hospitali mgonjwa wa mwisho wa Ebola. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliendelea kufuatilia hali hiyo ili kuhakikisha hakuna maambukizi yoyote ya virusi hivyo.