Wahamiaji waliofukuzwa na Trump na kupelekwa Afrika wasimulia sulubu walizokumbana nazo
-
Wahamiaji waliofukuzwa na Trump na kupelekwa Afrika wasimulia sulubu walizokumbana nazo
Wahamiaji kumi kutoka Marekani hadi Liberia wameliambia gazeti la The New York Times maelezo ya kutisha kuhusu miezi waliyotumia wakiwa kizuizini na safari ya saa 14 kwenda Afrika Magharibi, wakisema walipigwa, kufungwa minyororo na kutendewa vibaya, kabla ya baadhi yao kujikuta katika nchi ambazo hawana uhusiano nazo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Leonardo Sanchez, Mcuba mwenye umri wa miaka 49, alikuwa akipiga kelele kwa maumivu wakati wote wa safari ya kutoka Louisiana hadi Afrika Magharibi, baada ya maajenti wa Uhamiaji na Ushuru wa Marekani kumfunga pingu kwenye vifundo vya miguu na mikono na kuweka mnyororo kiunoni mwake uliomkandamiza tumboni ambako ana alama za majeraha ya zamani na upasuaji.
Sanchez ameiambia New York Times kwamba aliomba msaada wa kimatibabu mara kwa mara, lakini maafisa wa Marekani hawakumruhusu hata kutumia choo, na kumfanya ajikojolee.
Gazeti la New York Times limefichua kuwa ndege hiyo, ambayo ilibeba zaidi ya wahamiaji 40, ilikuwa ya kwanza katika mpango wa Marekani unaokusudia kutuma takriban watu 1,200 nchini Liberia ndani ya mwaka mmoja.
Haya yanafanyika kama sehemu ya sera ya utawala wa Trump ya kupanua operesheni ya kuwafukuza wahamiaji kwenda nchi zinazoitwa upande wa tatu, ikiwa ni pamoja na wale ambao wana amri za mahakama zinazowalinda wasirudishwe katika nchi zao.
Waliohamishwa katika operesheni hiyo wameliambia gazeti hilo kwamba wengi wao hawakujua wanakoelekea, na hofu hiyo ilitokea kwenye ndege wakati baadhi yao walipogundua kuwa huenda wanaelekea Liberia.
Watano kati yao wamesema walipigwa na maafisa wa uhamiaji wa Marekani, huku wengine wakisema walipigwa chini au kutwangwa makonde.
The New York Times inaripoti kuwa, baada ya kutua katika mji mkuu wa Liberia, Monrovia, Sanchez na wengine watatu walikataa kushuka, wakiogopa kuachwa katika nchi ya kigeni. Wamesema maafisa wa uhamiaji waliwalazimisha kutoka kwenye ndege, wakiwavua pingu zao kwa nguvu na kuwapiga chini, huku baadhi ya maafisa wakiwabana kwa magoti shingoni.
Gazeti hilo pia limeripoti ushuhuda kuhusu hali mbaya ya kizuizini nchini Marekani. Paula dos Santos, Mbrazili mwenye umri wa miaka 21, anasema alitumia miezi 15 katika vituo viwili vya kizuizini na alipitia kile alichokielezea kuwa ni kunyimwa huduma ya matibabu mara kwa mara.
Wahamiaji wengine wamesema walikuwa wakihamishwa mara kwa mara kati ya vituo tofauti, na kwamba baadhi yao waliwekwa katika vyumba vyenye baridi kali sana bila vitanda, ambavyo waliviita "majokovu," huku watu 50 wakishiriki choo kimoja.
Mwezi uliopita, Shirika la Amnesty International lililaani hatua ya Marekani ya kuwafukuza wahajiri na kuwapeleka huko Eswatini, ikiitaja operesheni hiyo kuwa ni "haramu." Ilikuwa ya nne ya aina hiyo na kuwahamisha wahajiri kwenda kwenye nchi hiyo ndogo ya kifalme ya kusini mwa Afrika tangu Julai 2025.