Watu 63 wafa wakati mgodi wa dhahabu ulipoporomoka huko Kordofan Sudan
Kwa uchache watu 63 wamepoteza maisha wakati mgodi wa dhahabu ulipoporomoka katika Jimbo la Kordofan, huko Magharibi mwa Sudan. Hayo ni kwa majubu wa taarifa ya leo Jumatano ya manusura na watu wa kujitolea.
Duru tatu za ndani zimetangaza habari hiyo kwa vyombo vya habari huku kundi moja la haki za wenyeji likisema kuwa, baadhi ya wachimbaji huenda bado wako hai chini ya ardhi na kuomba juhudi za haraka za uokoaji zifanyike.
Kikundi cha ufuatiliaji wa matukio mbalimbali cha Kordofan Observatory kimesema leo Jumatano kwamba zaidi ya wachimbaji 70 wa kienyeji walikufa au kutoweka baada ya mlolongo wa mashimo ya madini kuporomoka katika mgodi wa al-Zara wa eneo la Fouja la kaskazini magharibi mwa al-Nuhud.
Likinukuu maelezo ya mashahidi, kundi hilo limesema kuwa, manusura mmoja alitoka chini ya ardhi jana Jumanne na kuripoti kwamba wengine bado wako hai chini ya ardhi. Lilisema hakuna timu maalumu za uokoaji zilizoanzisha zoezi hilo kutokana na ardhi kuwa tepetepe, yenye mchanga ambayo inazuia majaribio ya wakazi wa eneo hilo ya kuwaokoa wachimbaji na kupata miili kwa kutumia vifaa vya kisasa.
Duru hizo tatu za ndani, zilipozungumza leo na vyombo vya habari zimesema kuwa kumeshuhudiwa idadi kubwa ya vifo katika eneo hilo la mbali kutokana na kukosekana taratibu za usalama na vifaa vya uokoaji.
Sudan ni moja ya wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika, lakini sehemu kubwa ya dhahabu yake huzalishwa kupitia uchimbaji hatari wa migodi isiyo na usalama wowote na baadaye husafirishwa nje ya nchi kwa njia ya magendo.
Uchimbaji wa dhahabu ni chanzo muhimu cha mapato kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vinavyopigana na Jeshi la Sudan, SAF.