Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na hali ya Sahara Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14863-umoja_wa_mataifa_watiwa_wasiwasi_na_hali_ya_sahara_magharibi
Umoja wa Mataifa umesema unatiwa wasiwasi na hali ya mambo katika eneo la kusini ya Sahara Magharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 08, 2016 03:29 UTC
  • Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na hali ya Sahara Magharibi

Umoja wa Mataifa umesema unatiwa wasiwasi na hali ya mambo katika eneo la kusini ya Sahara Magharibi.

Stéphane Dujarric,msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hali ya mambo katika eneo la Sahara Magharibi inatia wasiwasi na kubainisha kuwa umoja huo una wasiwasi wa kuanza tena mapigano kati ya vikosi vya usalama vya Morocco na Harakati ya Ukombozi wa Sahara Magharibi POLISARIO vilivyojizatiti kusini mwa eneo hilo na vilevile kutokana na uwezekano wa baadhi ya nchi za eneo kuingilia kati mapigano hayo.

Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa UN

Ameongeza kuwa licha ya jitihada za vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa Sahara Magharibi (MINURSO) vikosi vya pande mbili za Morocco na Polisario vimejizatiti kimapambano katika eneo la Guerguerat kutoka umbali wa mita 120 tu baina yao.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa MINURSO imeweka wasimamizi wa kijeshi wasio na silaha baina ya vikosi vya pande mbili na kwamba maafisa wa Umoja wa Mataifa nao wameshaanzisha mazungumzo na pande mbili pamoja na nchi zinazohusika katika kadhia ya Sahara Magharibi ili kutoa wito wa kuwepo uvumilivu na kutafuta ufumbuzi wa amani wa mgogoro huo.

Vikosi vya POLISARIO

Harakati ya kisiasa na kijeshi ya POLISARIO ya wananchi wa eneo la Sahara Magharibi inaendesha mapambano dhidi ya serikali ya Morocco ya kupigania kujitawala eneo hilo la kaskazini magharibi mwa Afrika.../