Ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji nchini Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15577-ukandamizaji_wa_polisi_dhidi_ya_waandamanaji_nchini_zimbabwe
Uepo mkubwa wa polisi katika mitaa ya mjini Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, umezuia kufanyika maandamano ya wapinzani dhidi ya serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 18, 2016 08:20 UTC
  • Ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji nchini Zimbabwe

Uepo mkubwa wa polisi katika mitaa ya mjini Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, umezuia kufanyika maandamano ya wapinzani dhidi ya serikali.

Viongozi wa muungano wa vyama vya upinzani wa serikali nchini humo walikuwa wamewataka wananchi kufanya maandamano makubwa siku ya Jumamosi ya terehe 17 ya mwezi huu. Muungano huo wa vyama vya upinzani, unataka kufanyika marekebisho ya sheria ya uchaguzi nchini Zimbabwe kabla ya kuwadia tarehe ya uchaguzi wa mwaka 2018, sanjari na kuondoka madarakani Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo. Rais Mugabeambaye pia ni kiongozi wa chama tawala cha ZANU-PF mwenye umri wa miaka 92, anakusudia kugombea tena kwa muhula wa sita katika uchaguzi ujao. Kabla ya hapo wiki iliyopita, serikali ilitangaza kupiga marufuku maandamano na mikusanyiko yoyote kwa kipindi cha mwezi mmoja, huku polisi ikitoa onyo kali dhidi ya kufanyika maandamano hayo katika kukaribia tarehe 17 Jumamosi iliyopita. Wakati huo huo, wanaharakati wa kisiasa na wapinzani wa serikali, wamekosoa vikali ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji mjini Harare, huku wakiituhumu polisi kutumia risasi hai katika kuwatawanya wafuasi wa muungano wa vyama vya upinzani katika maeneo matatu ya viunga vya mji mkuu huo wa Zimbabwe.

Waandamanaji dhidi ya serikali ya Mugabe

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, Rais Mugabe anatumia njia ya zamani ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani na ukatili na vitisho kwa ajili ya kuwanyamazisha wapinzani wake. Wakati huo huo, maelfu ya wafuasi wa upinzani walifanya manaandamo ya amani siku ya Jumamosi mjini Bulawayo, mji wa pili kwa ukubwa nchini Zimbabwe. Hii ni katika hali ambayo mahakama kuu nchini humo imewapa ruhusa wanaharakati wa kisiasa kufanya maandamano ya amani katika mitaa ya nchi hiyo. Ngarivhume mmoja wa viongozi wa upinzani wa Zimbabwe ambaye chama chake ni miongoni mwa muungano wa upinzani amesisitiza kwamba katiba na mahakama kuu kwa pamoja vimetoa idhini kwa wapinzani kufanya maandamano ya amani. Itakumbukwa kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2008, chama tawala cha ZANU-PF kiligawana madaraka na chama cha MDC chini ya uongozi wa Morgan Richard Tsvangirai. Ushindi wa kushangaza wa Tsvangirai katika uchaguzi, ulibua makelele ambayo yaliandamana na machafuko ambapo wafuasi wa chama cha upinzani waliuawa. Chama cha Tsvangirai pia kilifanikiwa kushinda viti 58 vya bunge na kwa kushirikiana na chama cha Arthur Mutambara kikaibuka na ushindi wa viti 101dhidi ya 90 vya chama tawala cha ZANU-PF.

 Arthur Mutambara mwanasiasa wa Zimbabwe

Ni kwa ajili hiyo ndipo kukajiri ugawanaji madaraka wa kihistoria nchini Zimbabwe. Hivi sasa, Rais Mugabe anakabiliana na mashinikizo ya kisiasa yanayomtaka kung'atuka madarakani. Hii ni katika hali ambayo mgogoro wa kiuchumi, ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira uliofikia asilimia 90 na upinzani wa kijamii kwa siasa za serikali yake,  vimeongezeka sana kiasi cha kuwafanya hata mashujaa wa vita vya ukumbozi wa Zimbabawe waliokuwa mstari wa mbele katika harakati za kupambana na ukoloni wa Mwingereza, kujiunga na safu ya upinzani dhidi ya serikali. Kujitenga askari hao wa zamani ambao walikuwa waungaji mkono wakubwa wa Rais Mugabe na chama tawala kumetajwa kuwa pigo kubwa kwa chama hicho. Hivi sasa, sanjari na ukandamizaji wa polisi dhidi ya wapinzani katika maandamano ya mjini Harare, muungano wa upinzani umetangaza maandamano makubwa ya nchi nzima katika wiki zijazo. Ni kwa kuzingatia hali hiyo , ndio maana weledi wa mambo wakatabiri kushtadi mivutano ya kisiasa nchini Zimbabwe katika siku za usoni.