Umoja wa Ulaya warefusha vikwazo kwa Spika wa Bunge la Libya
Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa, umemuongezea muda wa vikwazo Spika wa Bunge la Taifa la Libya.
Aguila Saleh, Spika wa Bunge la Libya na shakhsia wengine wawili wanatuhumiwa kuwa wanakwamisha jitihada za kurejesha amani nchini humo na kuacha kuiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Vikwazo hivyo vilianza kutekelezwa mwezi Aprili na mara hii vimeongezwa muda hadi Aprili mwaka kesho.
Vikwazo hivyo vinajumuisha marufuku ya kusafiri katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na vilevile kuzuia fedha za shakhsia hao katika Umoja wa Ulaya.
maafisa wengine wawilili kwa majina ya Khalifa al Ghawil ambaye ni kiongozi wa serikali ya Tripoli na Nouri Abu Sahmain, Mkuu wa Congresi iliyovunjwa ya Libya wamejumuishwa kwenye vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya.
Libya imekuwa na serikali mbili zinazopingana tangu katikati ya mwaka 2014. Muungano wa wanamgambo wa Libya uliudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli mwaka 2014 na kuasisi serikali.
Wakati huo huo serikali yenye makao yake huko Tobruk mashariki mwa Libya na inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mwezi Agosti mwaka huu ilishindwa kupata kura na uugaji mkono na Bunge la eneo hilo.