Feb 23, 2016 07:54 UTC
  • Ban Ki-Moon awasili Burundi, kukutana na Nkurunziza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewasili nchini Burundi katika kile kinachoonekana ni kujaribu kuupatia ufumbuzi mzozo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Ban Ki-Moon leo Jumanne anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Pierre Nkurunziza na viongozi wengine wa kisiasa nchini humo. Kadhalika anatazamiwa kufanya mazungumzo na asasi za kijamii na mashirika ya kutetea haki za binadamu. Safari ya Moon ambaye aliwasili Bujumbura jana, inajiri masaa machache baada ya watu wawili kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mripuko uliotokea viungani mwa mji huo mkuu. Aidha siku ya Jumapili, watu wawili waliuawa katika shambulizi lililotokea katika eneo la Gisozi mkoani Mwaro katikati mwa Burundi. Mkuu wa mkoa huo, Jean-Marie Nyakarerwa alisema kuwa hii ni mara ya nne kwa watu wenye silaha kufanya mashambulizi mkoani humo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita. Burundi ilitumbukia katika machafuko ya ndani baada ya kiongozi wa sasa wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea urais kwa mara ya tatu mfululiizo Aprili mwaka jana.

Tags