Polisi Burkina Faso waua magaidi katika makabiliano makali
Polisi nchini Burkina Faso wamempiga risasi na kumuua gaidi mmoja na wengine wawili wanasakwa baada ya ufyatulianaji risasi katika mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou.
Tukio hilo ambalo lililjiri mapema jana Jumapili ni la kwanza kushuhudiwa katika mji huo tokea magaidi wa kundi la Al Qaeda Eneo la Maghreb AQIM waliposhambulia Hoteli ya Splendid mwezi Januari na kuua watu 30. Walioshuhudia wanasema ufyatulianaji huo wa risasi ulikuwa baina ya polisi na kundi la watu katika mtaa wa Kilwin ambao wote walikuwa raia wa nchi hiyo. Mkuu wa Polisi ya Burkina Faso Lazare Tarpaga amesema, kuna msako mkubwa unaendelea kuhusu magaidi wawili waliotoroka.
Imedokezwa kuwa magaidi hao walikuwa wakiwasajili vijana kujiunga na makundi ya kigaidi yaliyoko kaskazini mwa nchi hiyo na eneo zima la Sahel.
Burkina Faso inapakana na Mali ambayo ina jangwa kubwa linalotumiwa na makundi kadhaa ya kigaidi yenye mfungamano na Al Qaeda na ISIS au Daesh.
Hayo yanajiri wakati ambao serikali ya Burkina Faso imetangaza kuwa imefichua na kusambaratisha njama za kutaka kuipindua serikali ya Rais Roch Marc Christian Kabore. Wafanyaji wa jaribio hilo wanawajumuisha waitifaki na shakhsia watiifu kwa Blaisse Compaore Rais wa zamani wa Burkina Fasso; ambao walikusudia kuipindua serikali ili kumrejesha madarakani.
Blaisse Compaore ambaye alisalia madarakani kwa miaka 27 alijaribu kuifanyia mabadiliko katiba ya Bukina Faso ili aendelee kuiongoza nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, lakini mwezi Oktoba mwaka 2014 alilazimika kujiuzulu kiti cha urais na kisha kukimbilia nchini Kodivaa kutokana na kupinduliwa na wananchi.