Burkina Faso yapitisha sheria inayoharamisha na kujinaisha mapenzi ya jinsia moja
Kikosi tawala cha kijeshi cha Burkina Faso kimepitisha sheria inayoharamisha mapenzi ya jinsia moja na kutangaza adhabu ya kifungo cha hadi miaka mitano jela kwa watu wote watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo hivyo vichafu. Wageni watakaopatikana na hatia pia watafukuzwa nchini humo kwa mujibu wa sheria hiyo mpya.
Sheria hii ambayo imekusudiwa kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vichafu vya mahusiano ya jinsia moja ilipitishwa kwa kauli moja na wabunge 71 wa bunge la mpito la Burkina Faso.
Kupitishwa sheria hii ni sehemu ya mageuzi mapana kuhusu sheria ya familia na uraia.
Vitendo vya ushoga vimepigwa marufuku katika nchi za Kiafrika karibu 30. Jirani ya Burkina Faso na muitifaki wake wa karibu Mali nchi ambayo pia inaongozwa na wanajeshi mwezi Novemba mwaka jana ilipasisha sheria kama hii.
Vitendo vya ushoga na ubaradhuli vimekuwa vikipingwa vikali huko Uganda na Ghana, nchi mbili ambazo katikamiaka ya karibuni zimeimarisha vikali sheria dhidi ya vitendo hivyo haramu.
Tangu washike hatamu za uongozi kupitia mapinduzi ya mwaka 2022, viongozi wa kijeshi wa Burkina Faso wameanzisha mageuzi makubwa ikiwa ni pamoja na kuakhirisha uchaguzi ambao uiltarajiwa kurejesha utawala wa kiraia nchini humo.