Ghana yakanusha kuwepo kambi ya wanamgambo wenye silaha kaskazini mwa nchi hiyo
Serikali ya Ghana imekanusha ripoti kwamba wanamgambo wanaobeba silaha huko Burkina Faso wanatumia eneo la kaskazini mwa Ghana kama kambi yao ya kuhifadhia zana za kijeshi na suhula za matibabu ili kuendeleza uasi na hujuma zao. .
Wizara ya Usalama ya Ghana jana ilitoa taarifa na kusema nchi hiyo haina sera ya uchokozi na haijafikia mapatano yoyote na makundi ya wanamgambo wenye silaha.
Wizara ya Usalama ya Ghana imekanusha vikali madai kuwa Ghana inatoa hifadhi kwa wanamgambo wenye silaha nakwamba vikosi vya usalama vya nchi hiyo vinapambana vikali dhidi ya ugaidi khususan kaskazini mwa nchi hiyo.
Taarifa ya Wizara ya Usalama ya Ghana imebainisha kuwa: Serikali ya nchi hiyo kupitia idara zake za usalama na intelijinsia zinaendesha oparesheni endelevu ili kuzuia kujipenyeza magaidi na wanamgambo katika maeneo ya mipakani; na imekuwa ikifanya hivyo kwa miaka kadhaa kwa mafanikio makubwa.
Ghana ina mpaka wa pamoja wa kilomita 600 na Burkina Faso, nchi ambayo ni kitovu cha vitendo vya ugaidi na mashambulizi ya wanamgambo wenye uhusiano na kundi la mtandao wa al Qaeda na kundi la Daesh. Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuhama makazi yao katika eneo la Sahel ,magharibi mwa Afrika.
