Machar aikosoa Kenya kwa kumtimua msemaji wake
-
Riek Machar
Kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini ameijia juu serikali ya Kenya kwa kumtimua nchini humo msemaji wake James Gatdet Dak na kusisitiza kuwa hatua hiyo imekiuka Hati ya makubaliano ya Geneva.
Machar ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini amekosoa hatua hiyo ya serikali ya Nairobi na kusema kuwa, mbali na kukiuka makubaliano hayo ya kimataifa, Kenya ambayo ni mdhamini wa Makubaliano ya Amani ya Juba, inahatarisha maisha ya mtu asiye na hatia.
Siku ya Jumatano, polisi nchini Kenya ilimkamata msemaji huyo wa Machar na kumzuilia katika kituo cha polisi cha uwanja wa ndege wa JKIA jijini Nairobi, kabla ya kumrejesha Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya siku ya Alkhamisi alisema taifa hilo halijuti kwa uamuzi wake wa kuwaondoa wanajeshi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki walioko Sudan Kusini chini ya mwavuli wa kikosi maalumu cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa (UNMISS) na kusisitiza kuwa, nchi hiyo itajiondoa kikamilifu katika mchakato wa kuupatia ufumbuzi mzozo wa Sudan Kusini.
Kenya ilitangaza kuwa itawaondoa wanajeshi wake walioko Sudan Kusini baada ya kamanda wake kutimuliwa kazini. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alimfuta kazi Luteni Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki baada ya ripoti ya uchunguzi kusema kuwa walinda amani waliokuwa chini ya jenerali huyo wa Kenya hawakuchukua hatua yoyote ya kuwalinda raia wakati wanajeshi wa serikali waliposhambulia kituo cha utoaji misaada mjini Juba, yaliyopzuka upya mapigano nchini humo Julai mwaka huu.