Kulaaniwa shambulio dhidi ya vikosi vya kimataifa kaskazini mwa Mali
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani shambulio dhidi ya msafara wa kikosi cha kimataifa cha kusimamia amani MINUSMA kaskazini mwa nchi ya Mali iliyoko magharibi mwa Afrika.
Ban Ki-moon amesisitiza kuwa, mashambulio dhidi ya walinda amani katu hayatadhoofisha azma walionayo wanajeshi hao ya kutekeleza majukumu yao ya kusimamia amani kaskazini mwa nchi hiyo. Askari watatu wa kusimamia amani nchini Mali waliuawa hivi karibuni kufuatia shambulio dhidi ya msafara wao.
Shambulio hilo lilifanyika sambamba na safari ya Waziri wa Ulinzi wa Canada huko nchini Mali. Harjit Sajjan Waziri wa Ulinzi wa Canada alielekea nchini Mali kwa shabaha ya kuchunguza suala la kutumwa askari 600 wa nchi yake katika nchi hiyo ya Kiafrika kwa lengo la kushiriki katika kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa MINUSMA.
Harjit Sajjan amesema, serikali ya Canada haina nia ya kufanya jambo la hatari kwa kutuma kikosi cha kusimamia amani nchini Mali na ndio maana kabla ya kuchukua uamuzi huo inahitajia muda zaidi wa kudurusu hatua hiyo. Maafisa wa Umoja wa Mataifa walielezea matumaini yao Januari mwaka huu juu ya kupelekwa kikosi cha kusimamia amani cha Canada katika eneo la kaskazini mwa Mali linalokabiliwa na hali ya mchafukoge. Ni kwa miaka mitatu sasa ambapo kuna polisi na wanajeshi 11 elfu wanaoshiriki katika kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa MINUSMA kaskazini mwa Mali.
Matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Canada juu ya kujiepusha na hatari inayoweza kujitokeza kutokana na kutumwa jeshi barani Afrika ni kinaya na ishara ya kutumbukia katika kinamasi Ufaransa kutokana na Paris kutuma wanajeshi wake barani Afrika. Januari mwaka 2013 Rais Francois Hollande wa Ufaransa alituma wanajeshi wa nchi yake kaskazini mwa Mali kwa madai ya kwenda kupambana na ugaidi. Majeshi ya Ufaransa yalipelekwa kaskazini mwa Mali kwa kisingizio cha kuikomboa kutoka katika udhibiti wa makundi ya kufurutu ada miji muhimu ya Timbuktu, Kidal na Gao. Makundi hayo ya wanamgambo yalizagaa katika maeneo ya mipaka ya Mali na Niger baada ya kuangushwa utawala wa dikteta wa Libya Kanali Muammar Gaddafi.
Licha ya kufurushwa akthari ya makundi yanayobeba silaha yenye uhusiano na kundi la kigaidi la al-Qaeda la Islamic Maghreb AQIM huko nchini Mali, lakini hadi sasa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa MINUSMA na wanajeshi wa Ufaransa hawana udhibiti wa maeneo mengi ya nchi hiyo.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kwa mara nyingine tena Ufaransa ina lengo la kupanua uwepo wake wa kijeshi nchini Mali kwa kutoa madai yasiyo na msingi ya kuenea ugaidi katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo na hivyo kujiweka katika mazingira mazuri ya kuweza kuyafutilia kwa karibu matukio ya Libya.
Licha ya kuweko uingiliaji wa kijeshi wa Ufaransa na vile vile kufikiwa makubaliano ya amani baina ya serikali ya Mali na makundi ya wabeba silaha mwaka 2015, lakini nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ingali inashuhudia vurugu na machafuko.
Katika upande mwingine, utendaji wa kikosi cha kimataifa cha kusimamia amani kaskazini mwa Mali unakosolewa na kukabiliwa na malalamiko kutokana na kuweko ripoti za vitendo vya ubakaji na utesaji raia vilivyofanywa na askari hao. Katika mazingira kama haya, serikali ya Mali sambamba na kukosoa maelekezo ya kiusalama ya Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, inataka isimamie jukumu la kudhamini amani na usalama wa kiwango fulani wa wananchi wa nchi hiyo; na kwa kupata ibra ya uingiliaji wa kijeshi wa Ufaransa mwaka 2013 izuie kuweko uwepo mkubwa wa kijeshi wa wananjeshi wa Ufaransa kaskazini mwa nchi hiyo.