Nov 29, 2016 07:05 UTC
  • UN yalaani machafuko Jamhuri ya Afrika ya Kati

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali machafuko ya hivi karibuni katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR)

Ban Ki-moon ametoa taarifa Jumatatu na kutaka makundi yanayohasimiana nchini humo kusitisha machafuko mara moja. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, katika kipindi cha wiki moja iliyopita, watu  85 wameuawa katika mapigano baina ya makundi ya watu wenye silaha na waasi wa Seleka katika eneo la Barya kaskazini mashariki mwa Bangui mji mkuu wa CAR.

Wakati huo huo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, imetajwa kuwa moja ya nchi masikini zaidi duniani. Hayo yamesemwa na, afisa wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA ambaye ameongeza kuwa nchi hiyo imesahaulika.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, mratibu wa masuala ya kibinadamu CAR Fabrizio Hochschild amesema nusu ya idadi ya watu CAR wanahitaji misaada ya kibinadamu, na hii ni kwa sababu ya vita vya muongo mzima vinavyoendelea na pia ukosefu wa utawala bora.

Askari wa UN wanaolinda amani CAR

Ameongeza kuwa, dola milioni 400 zinahitajika haraka kusaidia watu zaidi ya milioni moja na nusu ambao kati hao, milioni moja ni wale wanaorejea makwao baada ya kukimbia vita.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko na mapigano mwaka 2013 wakati makundi ya Kikristo yanayobeba silaha yalipoanzisha mashambulio yaliyoratibiwa dhidi ya kundi la Seleka lenye Waislamu wengi zaidi, ambalo mnamo mwezi Machi mwaka huo liliiondoa madarakani serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Francois Bozize. Hivi sasa kuna askari 10,000 wa kulinda amani katika nchi hiyo iliyo kati kati mwa bara la Afrika.

Tags