Touadera ashinda muhula wa 3 wa urais Jamhuri ya Afrika ya Kati
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin-Archange Touadera ameshinda muhula wa tatu urais, kwa mujibu wa matokeo ya awali ya uchaguzi wa karibuni, yaliyotangazwa Jumatatu na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchaguzi.
Touadera amepata asilimia 76.15 ya kura katika uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita, kwa mujibu wa matokeo hayo ya muda. Alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2016 na kushinda tena uchaguzi wa mwaka wa 2020 kwa kuzoa asilimia 53.16 ya kura katika duru ya kwanza.
Kura ya maamuzi ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ya 2023 iliondoa ukomo wa mihula, na kuongeza muda wa kuwa madarakani rais hadi miaka saba, hatua ambayo ilimuandaliwa Touadera uwanja wa kugombea muhula wa tatu.
Muungano mkuu wa upinzani, Kambi ya Republican ya Kutetea Katiba (BRDC), ulisusia uchaguzi huo, ukiuita kuwa si wa haki.
Waangalizi wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Afrika na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (MINUSCA), wamesema uchaguzi ulikidhi vigezo, licha ya ukosefu wa usalama kuendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya mashariki.
Profesa huyo wa zamani wa hisabati mwenye umri wa miaka 68 alifanya kampeni akitumia mafanikio ya serikali yake kurejesha usalama, na ushirikiano na wakandarasi wa usalama wa Russia na wanajeshi wa Rwanda anaosema ulisaidia kudhibiti tena eneo lililokuwa limetwaliwa na waasi, pamoja na kusaini mikataba ya amani hivi karibuni. Ushirikiano huo umeongeza ushawishi wa Moscow katika taifa hilo lenye utajiri wa madini, huku Russia ikistafidi na dhahabu, almasi, lithiamu na urani.
Washindani wa Touadera katika uchaguz huo akiwemo kiongozi wa upinzani na Waziri Mkuu wa zamani, Anicet-Georges Dologuele na Henri-Marie Dondra ambaye pia amewahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo walishutumu mamlaka kwa vikwazo vya kampeni, kama vile kuwazuia kusafiri kwenda kwenye majimbo.
Mahakama ya Katiba ina hadi Januari 20 kuidhinisha matokeo ya uchaguzi huo au kutoa uamuzi wa mapingamizi yoyote yatakayowasilishwa.