Wahajiri zaidi ya 200 waokolewa katika bahari ya Mediterania
Wahajiri zaidi ya 200 wamenusurika kufa maji baada ya kuokolewa katika bahari ya Mediterania.
Vikosi vya uokozi vya Umoja wa Ulaya jana Jumamosi vilifanikiwa kuwaokoa majini wahajiri 143 wakiwemo wanawake 5 na watoto 47 karibu na pwani ya Libya katika bahari ya Mediterania. Maafisa husika wa Uhispania pia wamesema kuwa wahajiri wengine 92 ambao walikuwa wakitaka kuelekea Ulaya wameokolewa majini karibu na pwani ya nchi hiyo katika bahari ya Mediterania; na kwamba wahajiri hao wamepelekwa katika bandari ya Malaga kusini mwa Uhispania. Maafisa hao wa Uhispania wameongeza kuwa wahajiri wengine 22 ambao walikuwa wamejificha ndani ya lori wakielekea katika mji wa Melilla gari lao lilisimamishwa na kisha wahajiri hao wakapelekwa katika kambi zilizopo katika mji huo. Hii ni katika hali ambayo Shirika la Msamaha Duniani Amnesty International lilitoa ripoti siku kadhaa zilizopita ikiikosoa miamala isiyo ya kibinadamu ya serikali ya Uhispania kwa wahajiri. Amnesty pia iliikosoa serikali ya Uhispania namna inavyoamiliana na wahajiri waliopo katika kambiza Melilla na Ceuta nchini humo.